*JUMLA YA ENEO LA EKARI MILIONI 13 ZINASHIKILIWA NA WATU SITA, AWATAKA WENYE LESENI ZA UTAFITI KUTOWATUMIA WACHIMBAJI WADOGO KAMA SEHEMU YA UTAFITI
Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde amemuelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, kufuta jumla ya maombi na leseni za Utafiti 2648 ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuomba na kuendeleza maeneo hayo kwa manufaa ya Taifa na ukuzaji wa Sekta ya Madini.
Waziri Mavunde amesema leo Machi 22, 2024 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kumekuwa na baadhi ya wamiliki wa leseni ambao wamekuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki wa leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura 123.
Miongoni mwa makosa ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara ni pamoja na wamiliki wengi wa leseni kutoanza au kutoendeleza maeneo ya leseni zao na badala yake kuhodhi maeneo; kutolipa ada stahiki za leseni.
“… kutowasilisha nyaraka muhimu kama Mpango wa Ushirikishwaji wa Watanzania Kwenye Shughuli za Madini (Local Content Plan), Mpango wa Wajibu wa Makampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility) na nyaraka za taarifa za fedha kuonesha matumizi yaliyofanyika pamoja na vielelezo vya matumizi husika.
“Ninatoa mfano kuna watu 6 tu wanahodhi maeneo yenye ukubwa wa ekari milioni 13 ukubwa wa maeneo hayo ni sawa na ukubwa mara nne wa Mkoa wa Kilimanjaro na hayafanyiwi chochote ili hali mahitaji ya maeneo ya uchimbaji ni mkubwa sana hapa nchini na hasa kwa wachimbaji wadogo ambao wamekuwa na mchango mkubwa sana kwenye kukuza sekta ya madini.
“Kuna watu wenye leseni za utafiti ambao hawatimizi masharti ya leseni zao na hivyo kutegea uwepo wa wachimbaji wadogo kama mgongo wa utafiti wao,” amesema Mavunde.
Amesema kutokana na kosa la kutolipa ada stahiki za leseni, kiasi cha takribani Shilingi bilioni 36 zinadaiwa kutoka kwa wamiliki na waliokuwa wamiliki wa leseni za utafutaji wa madini, leseni za uchimbaji mdogo wa madini na leseni za uchimbaji wa kati na mkubwa wa madini.
Kufuatia uwepo wa makosa hayo, Tume ya Madini imetoa Hati za Makosa kwa jumla ya leseni 59 hai kwa sababu wamiliki wake hawajatekeleza masharti na matakwa mbalimbali ya umiliki wa leseni husika.
Kutokana na hali hiyo imebainika kuwa wamiliki wa leseni, kumekuwa na baadhi ya waombaji wa leseni ambao wamekuwa wakitumia fursa ya uwepo wa teknolojia rahisi ya uwasilishaji wa maombi ya leseni – yaani mfumo wa Online Mining Cadastre Portal vibaya kwa kuwasilisha maombi mengi bila ya kulipa ada stahiki na wengine kuwasilisha maombi bila ya kuambatisha nyaraka zinazotakiwa kuwasilishwa pamoja na maombi ya leseni.
Katika uchambuzi uliofanywa na Tume ya Madini, imebainika kuwa, hadi Februari, 2024 kuna jumla ya maombi 2,180 ambayo hayajalipiwa ada stahiki za maombi.
Hata hivyo katika uchambuzi uliofanya na Tume ya Madini imebainika kuwa, hadi Februari, 2024 kuna uwepo wa maombi 409 ya muda mrefu ambayo wamiliki wake wamelipa ada za maombi lakini hawajawasilisha nyaraka muhimu zinazoambatana na maombi hayo.