Home KITAIFA NMB YAFUTURISHA DAR, WAZIRI MKUU AZITAKA SERIKALI ZA MITAA, TAASISI ZIJIFUNZE KWAO

NMB YAFUTURISHA DAR, WAZIRI MKUU AZITAKA SERIKALI ZA MITAA, TAASISI ZIJIFUNZE KWAO

Google search engine
Waziri Mkuuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia), akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede, wakati wa hafla ya Futari iliyoandaliwa na benki hiyo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha NMB, Juma Kimori. (Na Mpiga Picha Wetu).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, MKassim Majaliwa (kulia), akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya NMB, Dk. Edwin Mhede, wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na benki hiyo na kufanyika jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (kulia), akitoa mchango kwaajili ya maandalizi ya Futari kutoka kwa NMB kwa watoto wanaolelewakatika Kituo cha kulelea Watoto wanaoishi katika mazingira magumu cha Umrah Orphanage wakati hafla ya futari iliyoandaliwa na Benki ya NMB. Wa pili kulia ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya NMB, Juma Kimori. (Na Mpiga Picha Wetu).

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

 BENKI ya NMB imewafuturisha wateja wake walio kwenye Mfungo wa Mwezi Ramadhan Jijini Dar es Salaam, pamoja na kutoa misaada kwa vituo vya Watoto waishio katika mazingira magumu, huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiziagiza serikali za mitaa na taasisi za fedha, zijifunze kwa NMB namna ya kuwathamini wenye uhitaji.

 Hafla hiyo ya Iftar imefanyika Jumanne Machi 26, 2024 Jijini Dar es Salaam, ikiwa ni ya tatu kuandaliwa na Benki ya NMB tangu kuanza kwa ibada ya Funga ya Ramadhan ambayo ni nguzo ya pili kati ya tano za Dini ya Kiislamu, ikitanguliwa na hafla zilizofanyika katika Visiwa vya Unguja na Pemba, ambako pia kulitolewa misaada ya kijamii kwa watoto wenye uhitaji.

Waziri Mkuu Majaliwa alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya watu 1,200 wakiwemo wateja wa NMB, wadau, viongozi wa Serikali, Watoto wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu wa Vituo vya Al-zam (cha Mbagala), Umrah (Magomeni Mikumi) na Tanzania Kwanza (Tuangoma, Kigamboni).

Akizungumza mbele ya waalikwa hao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema NMB inastahili pongezi kwa namna inavyoyajali makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo kusapoti jitihada za elimu katika sekta za elimu, afya, maji, michezo na elimu za fedha kwa wajasiriamali.

“Leo hii nitapokea kutoka kwa NMB zawadi maalum kwa ajili ya Watoto wenye uhitaji wa vituo vya Al-zam, Umrah na Tanzania Kwanza vya Dar es Salaam. Kwa hili NMB mmefanya jambo kubwa sana, mnataka watoto hawa wajione kuwa wana thamani sawa na wengine.

 “Natambua kuwa licha ya kuwakumbuka watoto wenye uhitaji, mmekuwa pia mkichangia mahitaji kwenye shule zinazotumiwa na watoto wenye mahitaji maalum.

 “Pia, NMB ni benki inayoongoza kwa hutoaji huduma hapa nchini kwa sasa, ambayo imetenga kiasi cha Shilingi Trilioni moja  kwa ajili ya kuhudumia sekta ya kilimo nchini, hii ni kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye anakamilisha miaka mitatu ya uongozi wake madarakani,” amesema.

 Waziri Mkuu ameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa NMB ambayo ni benki ya ubiana Serikali ikiwa na hisa, ambapo imekuwa mnufaika wa hisa ilizonazo, akitolea mfano wa magawio makubwa, rekodi ikiwekwa mwaka 2023 ilikotoa gawio la Shilingi Bilioni 45.3 kwa Serikali, kiasi  ambacho hakijawahi kutolewa na mbia yeyote wa Serikali kama gawio.

Ametumia nafasi hiyo kuwapongeza watu wenye vituo vya Watoto Yatima na Watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu na kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kimaendeleo katika umri wao na kwamba NMB inaongoza njia inayopaswa kupitwa na taasisi nyingine kiasi cha kutaka ziige mwenendo huo.

 “Kama ambavyo nimetoa wito kwa taasisi na wadau wengine kuiga kwa NMB, Nitumie fursa hii pia kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa,  ambazo ni taasisi ya Serikali, wastahiki mameya mpo hapa, wakuu wa wilaya mpo hapa, madiwani wachache wawakilishi mko hapa, lichukueni hili kama ajenda.

“Hakikisheni watoto hawa walemavu, yatima, wanaoishi mazingira magumu na wenye mahitaji maalum, wasiwe wanafikiwa tu kipindi cha Ramadhan, iwe ni utaratibu wa kila siku katika maisha yao yote. Halmashauri ziratibu mwenendo wao, mahitaji yao, huduma zao, ili watoto hawa tuwalee.

“Hawa ndio Watanzania ambao baadaye watakuwa viongozi wa taifa hili, kwahiyo Mamlaka za Serikali za Mitaa, jifunzeni kutoka kwa NMB, namna ya kushiriki kikamilifu kutambua vituo na kuvihudumia,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Meya wa Dar es Salaam, Omar Kumbilamoto.

 Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, alitoa salamu za shukrani kwa Waziri Mkuu kwa kuhudhuria hafla hiyo, akiwashukuru pia wateja, wadau na viongozi wote waliotikia mwaliko wa taasisi yake kujumuika pamoja.

“Katika kila Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, tumekuwa na utamaduni huu wa kupata futari ya pamoja na wateja wetu, wadau, viongozi na waalikwa wengine kama ishara ya upendo, umoja, mshikamano. Ujio wenu nyinyi wote unathibitisha kuwa nyie ni familia ya NMB.

 “Pamoja na futari hii, lakini mwaka huu tutakabidhi misaada kwa watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu. Tuna vituo vitatu hapa vyenye watoto takriban 200, ambavyo tunaenda kuvipa zawadi za mfungo ili wakitoka hapa wakaendelee kuufurahia mwezi wa Ramadhani na Sikukuu ya Idd,” amebainisha Kimori.

 Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, amesema umuhimu wa majumuiko ya namna hiyo ni kujenga jamii ya watu wenye Hofu ya Mungu, watu ambao wanahitajika sana katika kukuza Uchumi wa Nchi na ustawi wa taasisi kama NMB.

“Afisa Mkuu wa Fedha tayari ameshazungumza kwa kina, kwamba pamoja na ibada ya futari, NMB inaenda kuwashika mkono wahitaji ambao tumeambatana nao hapa. Wito wetu kwa jamii ni kuendelea ‘kubenkika’ na NMB inayotumia kaulimbiu ya Karibu Yako, ili kutanua familia hii,” amesema Dk. Mhede.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here