*MONGELA, MAKALA, KUPANGIWA KAZI NYINGINE, MA-DC, MANAIBU KATIBU WAKUU WAGUSWA
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
NI Usiku wa mabadiliko. Ndivyo unaweza kusema, wakati Watanzania nchini wakiungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, hali imekuwa tofauti kwa aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Profesa Joyce Ndalichako, ambaye ametupwa nje kwa utenguliwa kwenye uteuzi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo inatajwa kuwa ni sehemu ya mabadiliko ya kawaida ndani ya Serikali huku macho na masikio yakisubiri Aprili 4, 2024 wakati wa uapisho wa viongozi wateule huenda Mkuu wa nchi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akaweka wazi sababu ya mabadiliko hayo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa usiku huu wa Machi 31, 2024 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus, ilieleza kuwa Rais Samia amefanya uteuzi, utenguzi na uhamisho wa vingozi kadhaa.
Katika panga pangua ya safari hii, imemgusa Mbunge wa Kasulu Mjini, Profesa Joyce Ndalichako, akiwa ni Waziri pekee ambaye ameguswa na panga hilo na kuwekwa kando na nafasi yake kuchukuliwa na Deogratius Ndejembi ambaye sasa anakuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) huku mtangulizi wake akitenguliwa.
Ndejembi ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) katika rekodi inaonyesha kuwa pia alikuwahi kuwa Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, sasa amekabidhiwa kijiti hicho akiwa na uzoefu na sura hali ya utumishi nchini ikiwamo sekta ya ajira.
MAKONDA ‘IN’ ARUSHA
Katika panga pangua hiyo, Rais Samia ameteua aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya John Mongela, ambaye atapangiwa kazi nyingine.
Makonda pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa utawala wa Serikali ya Awau ya Tano chini ya Rais hayati Dk. John Magufuli
Mbali na hilo panga hilo pia limewagusa waliokuwa wakuu wa mikoa ya Mwanza (Amos Makala) huku nafasi yake akipelekwa Said Mtanda, ambaye awali alikuwa Mara na John Mongela ambaye nafasi yake amepelekwa Makonda.
Pamoja hilo katika uteuzi huo, safari hii imeibua manaibu waziri wawili wapya akiwamo Mbunge wa Viti Maalum, Zainab Athuman Katimba ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI akichukua nafasi ya Ndejembi pamoja na Mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo ambaye naye ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akichukua nafsi ya Jumanne Sagini ambaye amepelekwa Wizara ya Katiba na Sheria kuwa Naibu Waziri.
KAULI YA RAIS SAMIA
Machi 13, 2024 Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza kwenye hafla ya kuwaapisha Viongozi wateule leo tarehe 13 Machi, 2024 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Ikulu jijini Dar es Salaam aliweka wazi siri ya panga pangua yake ndani ya Serikali.
“Wale wanaoji-identify huyu wa Mama. Mimi Mama nina watoto wote. Anaefanya vizuri wangu na anaefanya vibaya wangu. Mwingine nitampa zawadi ukinifanyia vibaya nitakuchapa mikwaju. Wapo ninaowachapa mikwaju nawuweka nje kidogo akishapata adabu yake namwambia njoo tufanye kazi,” alisema Rais Samia katika hafla hiyo.
SOMA KWA UNDANI TAARIFA YA UTEUZI