*MAKONDA ANUSA DALILI KABLA MKEKA WA RAIS SAMIA, LUKUVI, BULEMBO NAO ‘WAGUSWA’
Na MWANDISHI WETU
-BEST MEDIA, DAR ES SALAAM
WAKATI macho na masikio ya Watanzania wakiwamo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakitafakari namna Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Samia Suluhu Hassan namna atakavyosuka safu mpya baadhi ya makada wa CCM wanatajwa kwenye uteuzi wa nafasi nyeti.
Hatua hiyo imekuja saa chache baada ya Rais Samia kuwateuwa watendaji wa chama hicho akiwamo aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha huku makatibu wa jumuiya za vijana na wazazi za CCM wakiteuliwa kuwa wakuu wa wilaya jambo linalotoa nafasi kwa kujazwa kwa nafasi hizo ndani ya chama.
Kutokana na hali hiyo taarifa kutoka ndani ya CCM zinaeleza kuwa wakuu wa mikoa walioachwa kwenye uteuzi huo, Amos Makalla pamoja na John Mongela wanatajwa na kuewa nafasi kubwa ya kurudishwa kwenye nafasi za ndani ya chama kama mkakati wa Rais Samia wa kusuka safu mpya kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Chanzo cha kuaminika kutoka Makao Makuu ya CCM Jijini Dodoma, kiliambia Best Media leo kuwa baada ya Aprili 4, 2024 kuapishwa kwa viongozi walioteuliwa na Rais Samia, kikao cha Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya dharura kitaitishwa na kupelekewa mapendekezo ya majina ya makada wa chama hicho kwa mujibu wa utaratibu wa CCM.
Wanaotajwa kurithi nafasi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Anamringi Macha ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla.
Hatua hiyo ambayo imetoa nafasi wazi baada ya Macha kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, akichukua nafasi ya Christina Mndeme ambaye naye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), katika mabadiliko hayo yalifanyika Machi 12, 2024.
“Wengine ambao majina yao yanatajwa kenye uteuzi huu ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela ambaye anatajwa huenda akapelekwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana akichukua nafasi ya Fakii Lulandala ambaye ameteuliwa Mkuu Mkuu wa Wilaya Simanjiro Mkoani Manyara,” kilisema chanzo hicho
Hata hivyo kwa nafasi ya Katibu wa Siasa na Uenezi, wanaotajwa kuchomoza najina yao ni washauri ya Rais, Abdallah Bulembo pamoja na William Lukuvi ambapo huenda mmoja wao akaingia kuvaa viatu vya Makonda ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa miezi mitano nalo jina la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nalo limekuwa likitajwa kwenye orodha ya kumrithi Makonda.
“Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi kuna nafasi kubwa Katibu Mkuu atatoka upande wa Zanzibar kwa maana Mwenyekiti ametoka uapnde wa Bara, katika ile kuleta uwino katika suala la Muungano,” amesema
MAKONDA ANUSA KABLA
Akiwa Wilayani Tarime katika mazishi ya aliyekuwa mke wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Christopher Gachuma, Makonda alikuwa ni miongoni waliohudhuria shughuli hiyo ya mazishi katika muonekano alikuwa mnyonge na alijitenga hata kukaa jukwaa kuu.
“Jana kwenye mazishi ya mke wa Gachuma, Makoda alikuwa mnyonge sana, hata alipofika hakuwa na kundi la wapambe kama kawaida yake. Alipofika msibani alitusalimia na kukaa pembeni kama waombelezaji wengine na hakwenda kuketi jukwaani walipokuwa viongozi wenzake.
“Nahisi alishapata taarifa kabla maana si kawaida yake kuwa kwenye muonekano wa uonyonge namna ile,” alisema mmoja wa kiongozi wa CCM ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake