Na MWANDISHI WETU
-MKURANGA
BALOZI wa Heshima wa Shelisheli nchini Tanzania, Maryvonne Pool kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas, wamegawa mitungi ya gesi 400 kwa wanawake wa Kata ya Mwalusembe wilayani Mkuranga huku wakihimizwa kutunza mazingira kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mitungi hiyo Balozi Maryvyonne Pool ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya African Reflections Foundation, amesema kuwa uamuzi wa kushirikiana na Oryx kutoa mitungi hiyo kwa wanawake wa vijiji vya kata vya Mwalusembe, unatokana na kutambua na kuunga mkono jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha nishati safi ya kupikia.
“Hii kwangu si mara ya kwanza kwani mwaka 2022 nilinunua mitungi ya gesi na kugawa kwa wanawake wa Mkuranga kwa sababu mimi ni balozi wa heshima hapa Mkuranga.
“Ndio maana nimekuwa nikishiriki katika miradi ya maendeleo ukiwemo wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji,” amesema
Kutokana na hali hiyo, amesema kuwa taasisi yake imekuwa ikiwasidia wanawake na vijana kulima, huku akibainisha kuwa hatua hiyo imetokana na kutambua mchango wa Rais Dk. Samia baada ya kuwa ‘Champion’ wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
“Kulifanyika mkutano wa mazingira wa kimataifa uliofanyika Dubai ambapo Rais Samia alichaguliwa kuwa champion wa kuhamasisha nishati safi ya kupikia , hivyo ni vema kumuunga mkono Rais Samia katika ajenda hiyo.
“Katika ule mkutano nilikaa meza moja na Rais (Dk.Samia) pamoja na Bilionea wa Marekani Bill Gate ambapo Rais Samia alichaguliwa kuwa champion wa Afrika katika kuhamasisha nishati safi, hivyo anastahili pongezi na nimeahidi kuunga mkono na kumsaidia kadri nitakavyoweza,”amesema Balozi Pool.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Rufiji ambaye pia anakaimu nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Meja Edward Giwele, amesema umefika wakati wa kumuunga mkono kwa vitendo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuokoa mazingira na kutanua fursa za kiuchumi hususan kwa wanawake wa wilaya hiyo nan a maeneo mengine nchini.
“Leo tumegawa mitungi ya gesi 400 kwa wanawake wa kijiji cha Kinene katika kata ya Mwalusembe ndani ya wilaya Mkuranga ikiwa sehemu ya mwendelezo wa jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha tunatumia nishati safi au nishati mbadala na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa,” amesema DC Meja Gowele
Ameeleza kuwa, azma ya Rais Samia ni kutunza mazingira katika maeneo yote.
“Nitumie fursa hii kumpongeza mwakilishi wa Oryx na Shirika la Afrika Reflections Foundation kwa kushirikiana na kuhakikisha wanagwa mitungi hiyo kwa akinamama tena wa hali ya chini kabisa katika kijiji hiki cha Kinene.
“Mwito wangu kwao ni lazima tuhakikishe tunasimamia yale maelekezo ya Rais ya kutunza mazingira lakini tunaacha matumizi ya kuni na mkaa badala yake tutumie gesi ambayo ni safi na salama kwa ajili ya matumizi ya kupikia,” amesema.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mwakilishibwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania, Janeth Mutashobya, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa azma yao ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Aidha amesema Kampuni ya Gesi ya Oryx itaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za akinamama na jamii kwa ujumla na kwamba kupika kwa gesi ya Oryx ni kulinda mazingira kwa kuacha kukata miti.
“Pia ni kulinda afya ya wanawake kwa kuwaepusha kuvuta moshi na mvuke unaoathiri mapafu na afya yao unaotokana na kuni na mkaa,” amesema.
Mutashobya amesema kuwa kwa miaka mingi Oryx Gas imekuwa kampuni kiongozi katika kukuza matumizi ya Gesi nchini Tanzania na kuanzia Julai mwaka 2021 wamekuwa mstari wa mbele kutekeleza maelekezo ya Serikali waliyopokea toka kwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ifikapo mwaka 2023 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga, Omar Mwanga amesema changamoto kubwa waliyonayo ni uharibifu wa misitu ambao unatokana na ukati miti kwa ajili ya kuchoma mkaa,hivyo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanakuwa walinzi wa misitu sambamba na kutumia nishati safi ya kupikia.
Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa wahanga wa uharibifu wa mazingira.
Hata hivyo amesema kuwa misitu mingi ya asili imekatwa mkaa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuwivisha chakula.