NA MWANDISHI WETU
-DODOMA
WIKI moja tangu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoipongeza Benki ya NMB kwa jicho la huruma kwa Watoto Yatima, na kuzitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Fedha kujifunza kwao namna ya kuwafikia na kuwasaidia wenye uhitaji, Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, naye amekiri kuvutiwa na ibada hiyo.
Machi 26, Waziri Mkuu Majaliwa aliipongeza NMB kwa aina mpya ya ufuturishaji wateja wao waliofunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, wadau na viongozi wa Serikali, inayoenda sambamba na utoaji misaada kwa Watoto Yatima na Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu, na kutaka kuwepo mpango mkakati uliobeba maono kama hayo.
Utaratibu huo mpya wa ufuturishaji, ulianzia visiwani Zanzibar, ambako NMB ilikabidhi misaada ya vyakula, mafuta ya kupikia, sukari, sabuni na vifaa vingine kwa vituo vya Kidundo na Mazizini Orphanage, kisha kuendelea ilipofuturisha jijini Dar es Salaam, ilikovisaidia vituo vya Umrah, Tanzania Kwanza na Al Zam.
Akizungumza wakati wa Iftar iliyojumuisha Viongozi wa Serikali, Wabunge wa Bunge la Tanzania, wateja, wadau na Watoto Yatima wa Vituo vya Zam Zam na Darul Maarifu vya jijini Dodoma, Spika, Dk. Tulia ambaye ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, alisema NMB imefanya ibada kubwa kuwashika mkono Watoto hao katika kipindi cha Ramadhan.
“Niwapongezea kwa sadaka hii, ambayo mmenitaka mimi kuwakabidhi watoto hawa Afisa Mkuu wa Fedha ameeleza hapa maeneo mbalimbali mlikopita kufuturisha na kusaidia jamii ya wenye uhitaji, viongozi wa serikali na wateja wenu, tunawapongeza kwa sababu mmeenda kuwafuturisha wapiga kura wetu huko.
“Tunaithamini sadaka hii, tunawapongeza NMB kwa kazi nzuri, na hii ni kwa niaba ya wote waliofuturu hapa na ambao hawawezi kupata fursa ya kuongea, naomba mfahamu tu kuwa tunaheshimu sana sadaka hii mliyoitoa leo hapa na kule kote mlikofuturisha.
“Tunawashukuru sana NMB, kwakweli mnafanya vizuri na tunawapongeza sana sana, kwa kuwa hii ni taasisi ya kifedha, inayofanya kazi za maendeleo. Tunawapongeza kwa mchango mkubwa wa maendeleo ya taifa mnaotoa kwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan,” alibainisha Spika, Dk. Tulia.
Akinukuu Qur ani Tukufu Surah ya 99 (Az Zalzalah), aya ya saba hadi ya nane – (inayosema; Basi yule mwenye kutenda wema mdogo mfano wa mdudu chungu, atalipwa na mwenye kutenda uovu/ubaya mdogo mfano wa sisimizi, atalipwa), Spika Tulia aliitabiria mafanikio makubwa NMB kwa ukubwa wa ibada za kijamii inazofanya.
“Ni matumaini yetu kuwa kwa kazi nzuri mnayofanya, ikiwemo kujali na kuthamini haya makundi maalum, mafanikio yenu yatakuwa makubwa zaidi na miaka ijayo tutashuhudia hafla hizi majimboni ama mikoani, kwa sababu Allah atakuongezeeni mafanikio kutokana na ibada zenu za kuwajali watoto hawa.
Awali, Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, ambaye alimwakilisha Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Ruth Zaipuna, alisema ufuturisha wateja, waumini na wadau wao umekuiwa wa muda mrefu, lakini mtazamo chanya kwa jamii ukawasukuma kufikiria kufanya kitu kwa makundi ya wenye uhitaji.
“Kila mwaka huwa tunafanya hafla hizi, lengo likiwa kudumisha ukaribu na kustawisha mahusiano mem ana jamii inayotuunga mkono, lakini namna ya kipekee mwaka huu tumekuwa tukialika watoto kutoka katika vituo vya wenye mahitaji maalum na kuwasaidia, leo tukiwa na takribani watoto 100 kutoka vituo vya hapa Dodoma.
“Tunaamini kwamba hii ni fursa ya watoto hawa kujifunza na kuendelea kuhamasika kutenda mema na kuwa wakarimu kwa jamii. Ndio kusema leo hatutoishia tu kufuturisha, bali tutawasaidia watoto wa Vituo vilivyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), vya Zam Zam na Darul Maarifu vya hapa Dodoma,” alibainisha Kimori.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Dk. Edwin Mhede, alimshukuru Spika Tulia kwa kuhudhuria hafla hiyo na kwa niaba ya Bodi, wanamshukuru yeye kutenga muda wa kujumuika nao, huku akisema NMB na Bodi kwa niaba ya wanahisa wanawashukuru pia waalikwa wote na ujio wao ni ishara kwamba wana mashirikiano mema na wadau.
“Na kwenye mashirikiano mema, kuna kuelimishana, kukosoana ili kujengana kwa nia ya kufanya vizuri zaidi na katika mkutano huu wa ibada, hatutaacha kupokea maoni na mrejesho kutoka kwenu ili kutusaidia tuweze kuimarisha oparesheni zetu na huduma kwa wananchi na sekta tunazozihudumia kila siku.
“Ukiachana na ukweli kwamba hii ni ibada, lakini kwanini tunakutana? Kitabu Kitukufu cha Qur ani kinatuasa na kutuhimiza umuhimu wa kukutana na kukumbushana, kwani inaaminika kwamba katika kukumbushana, ndiko tunakoweza kujengana vizuri kabisa. Kwa hiyo kusanyiko hili ni la Kimungu na lina baraka zote,” alifafanua Dk. Mhede.