Home KITAIFA WANAWAKE MIRERANI WAANDAMANA KUPINGA KUFUNGWA  MIGODI

WANAWAKE MIRERANI WAANDAMANA KUPINGA KUFUNGWA  MIGODI

Google search engine

Na MWANDISHI WETU

-MIRERANI, MANYARA

WANAWAKE ambao wanafanya kazi ya kuchekecha michanga katika Machimbo ya Tanzanite Mirerani wanaofanya biashara za madini wameandamana kumuomba Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kuingilia kati mgogoro wa kufungwa baadhi ya  migodi ya wachimbaji wadogo.

Wanawake hao wameyasema hayo Aprili 9, 2024 kutokana na hatua ya kufungwa kwa njia za migodi hiyo, ikiwepo migodi wa Saniniu Laizer ambao  hadi sasa unashikilia rekodi ya kutoa madini makubwa lakini pia kulipa kodi kubwa kwa serikali umewasababishia umasikini na kushindwa kumudu familia zao.

Sambamba na njia ya mgodi huo,pia migodi mingine ya wachimbaji wadogo imefungwa na baadhi kulazimishwa kuingia ubia ya Franone ili waweze kuendelea kuchimba madini.

Hellena Daud mchekechaji wa madini amesema kufungwa kwa migodi ya wachimbaji wadogo kumepelekea kuwa na gali ngumu zaidi kwao kwani kwa sasa wanapata udongo kwa shida wanaweza kushinda kutwa na wasipate chochote cha kurudi nacho nyumbani.

Naye Ummy Rajabu Chandu mchekechaji wa madini ameungana na mwenzake kwa kusema kuwa kufungwa migodi wa wachimbaji wadogo kumeathiri uchumi na ajira za akina mama .

Akizungumzia athari hizo mfanyabiashara wa madini mjini Mirerani, Herieth Evarist Mushi, amesema kuwa wameshindwa kuwapeleka watoto shule baada ya mji wa Mererani kufa kwani watu hawana ajira na wamekosa madini kutokana na madini yote kuhodhiwa na Kampuni ya Franone ambayo imekodishiwa eneo la Kitalu C.

Kutokana na hali hiyo, amesema kuwa shughuli zote za  uuzaji wa madini ndani ya ukuta Mirerani umbali wa kilomita tisa ambapo gharama za usafiri kwenda na kurudi ni Shilingi 6,000 kwa pikipiki kila siku kumeongeza ugumu wa maisha yao.

Lightness Daniel mkazi wa Mirerani amesema kuchukuliwa njia za madini kwa wachimbaji wadogo kutapelekea kukosekana kwa ajira kwa kundi kubwa la watu wengi.

“Migodi ya wachimbaji wadogo ambayo imefungwa ndio hutoa fursa ya ajira nyingi kwa vijana na kuwapa udongo  wanawake,” amesema

Lightness  amesema kuwa udongo ambao walikuwa wakipata ndio huchekecha na kujipatia madini ambayo huyauza na kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao.

“Lakini pia tunamuomba Rais Samia aruhusu  biashara ya madini kufanyika katika mji wa Mirerani na pia wale waliofungiwa waachiliwe kwani huwarahisishia kujipatia kipato na ajira za uhakika,” amesema Liana Mlay ambaye ni mfanyabiashara anayetembeza bidhaa za nyumbani Kwa kutumia mkokoteni

Ritha Steven Siliwimba , brocker wa madini amesema kuwa Saniniu Laizer alikuwa akitoa msaada wa mchanga na fedha  kwa wanawake wengi wa Mirerani lakini tangu njia yake kuvamiwa anashindwa kutoa udongo wa kutosha na kusababisha wapate shida.

Naye Ritha alidai kuwa Kampuni  ya Franone hatoi ajira kwa wazawa wa Mirerani na hivyo kusababisha ukosefu mkubwa wa ajira

Gladness Godfrey Mingi, amesema kuwa njia za madini zimekatwa na kwenda kwa Mwekezaji wa Kitalu C  Franone na hivyo kupelekea kukosekana kwa ajira za kudumu kwa wakazi wa Mirerani kwani yeye Franone hajajiri wakazi wa Mirerani.

Wakizungumzia mgogoro wa Mirerani , Waziri wa Madini Anthony Mavunde na Mkuu wa mkoa Manyara Queen Sendiga wametaka busara kutumika kumaliza migogoro ya Mirerani.

Waziri Mavunde amesema Serikali haitaki kuona Mirerani inakuwa na vurugu lakini pia Kuna wachimbaji wanahujumiana.

Amesema kuwa wizara yake pia imekamilisha zoezi la kupiga picha eneo lote ya migodi ya Tanzanite ndani ya ukuta na nje ili kuona akiba ya madini iliyopo.

“Baada ya taarifa kutoka tutawapa lakini maono yangu Mimi ipo siku Mirerani itakuwa haina mgogoro hata mmoja,” amesema Waziri Mavunde

Naye Mkuu Mkoa Manyara, Queen Sendiga pia ametaka busara kutumika Mirerani ili kumaliza migogoro.

“Kila mtu lazima akubali kupoteza kitu ili kutatua migogoro hapa Mirerani,” amesema

Katika machimbo hayo mgogoro mkubwa ni sheria ya uchimbaji madini ya vito ambayo inataka mchimbaji kuchimba madini katika eneo lake la lesseni tu kwenda chini.

Hata hivyo wachimbaji wanapinga sheria hiyo kwani Madini ya Tanzanite wanachamba kwa kufuata miamba ya Madini na mingi inaelekea kitalu C ambacho amepewa mwekezaji mmoja ambaye ni Kampuni ya Franone .

Katika Machimbo ya Mirerani kuna zaidi ya migodi 400 katika kitalu A,B,D  lakini kitalu C Kuna Mwekezaji mmoja.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here