Home MAKALA NMB ILIVYOACHA ALAMA MIOYONI MWA YATIMA, WENYE UHITAJI KUPITIA IFTAR YA RAMADHAN...

NMB ILIVYOACHA ALAMA MIOYONI MWA YATIMA, WENYE UHITAJI KUPITIA IFTAR YA RAMADHAN 2024

Google search engine

•VITUO SABA ZANZIBAR, DAR ES SALAAM, DODOMA VYENYE WATOTO ZAIDI YA 1,000 VYAPEWA MISAADA

•MAKAMU WA PILI WA RAIS SMZ, WAZIRI MKUU JMT, SPIKA WA BUNGE WAIPONGEZA, WANUFAIKA WAFUNGUKA

NA MWANDISHI MAALUM

KUFUTURISHA wateja wake walio kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, umekuwa ni utamaduni endelevu kwa Benki ya NMB.

Kila mwaka, katika kila kipindi cha utekelezaji wa ibada ya funga, ambayo ni Nguzo ya Pili kati ya tano za Kiislamu, NMB kupitia Programu ya Uwekezaji kwa Jamii (CSI – zamani CSR), imewakutanisha pamoja wateja wao pamoja na wadau wengine wakiwemo viongozi wa Serikali.

Ni kupitia hafla hizo za Iftar, NMB huwaweka pamoja wateja wao kutafakari maadili yanayounganisha binadamu wote, upendo kwa familia zao, shukrani kwa Mwenyezi Mungu, lakini pia toba na kuzidisha ushirikiano katika ibada.

Katika hafla ya kwanza, mjini Unguja, Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa NMB, Ruth Zaipuna alisema: “Umekuwa ni utamaduni endelevu wa NMB kuandaa futari katika kipindi hiki cha Ramadhani na mara zote tumekuwa tukialika wateja wetu, wadau na wageni wengine katika futari hizi.

“Pamoja na kuwaalika wateja wetu, viongozi na wadau mbalimbali, leo pia NMB imetumia fursa hii kujumuika na watoto kutoka katika Vituo vya Yatima na Wanaoishi kwenye Mazingira Magumu, ambao wameungana nasi na watapokea misaada mbalimbali.

“Sisi NMB tunaamini kuwa, uwepo wa watoto hawa ni fursa ya wao kujifunza na kuendelea kuhamasika katika kutenda mema na kuwa wakarimu kwa jamii inayowazunguka. Tunawasihi watoto hawa waendelee kukua katika Imani, wamtegemee Mwenyezi Mungu na wazidishe juhudi maishani, Mungu atawasaidia,” alisema Zaipuna.

MISAADA KWA WENYE UHITAJI

Katika Ramadhan ya mwaka huu wa 2024, utaratibu huo uliongezwa thamani na NMB, ambako ilizitumia hafla hizo kuwaalika Watoto Yatima na Wanaoishi Kwenye Mazingira Magumu, kufuturu nao pamoja, kisha kuwapa misaada mbalimbali ya kijamii kwa ajili ya muendelezo wa funga zao na Sikukuu ya Eid el Fitr.

Zaidi ya watoto 500 walihudhuria hafla mbalimbali za NMB Iftar zilizofanyika Unguja, Pemba, Dar es Salaam na Dodoma, huku misaada waliyopewa ikienda kugusa zaidi ya watoto 1,000 walio kwenye vituo saba vilivyonufaika na bidhaa za mamilioni ya shilingi walizopewa na NMB.

 Mjini Unguja, Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ, Hemed Suleiman Abdulla, alipokea misaada hii kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu (CEO), wa NMB, Ruth Zaipuna, kisha naye kuikabidhi kwa viongozi na walezi wa vituo vya Kidundo Orphanage Center na Mazizini Orphanage Center vya Zanzibar.

Ilikuwa hivyo pia jijini Dar es Salaam, ambako Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, alipokea misaada mbalimbali ya kijamii kutoka kwa Afisa Mkuu wa Fedha, Juma Kimori, kabla ya Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali Bungeni kuikabidhi kwa wenye uhitaji kutoka Tanzania Kwanza Orphanage, Al Zam Orphanage Center na Umrah Orphanage Center.

Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson Mwansasu, naye akaingia katika orodha ya viongozi wakuu wa Serikali aliyepokea misaada ya NMB, wakati wa Iftar bungeni, kisha naye kuikabidhi kwa viongozi wa watoto wanaolelewa na Zamzam Islamic na Darul Maarifa, vituo vilivyo chini ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) – Jiji la Dodoma.

KAULI YA MAKAMU WA RAIS SMZ, WAZIRI MKUU, SPIKA WA BUNGE

“Kwa hili NMB mmefanya jambo kubwa sana, mnataka watoto hawa wajione kuwa wana thamani sawa na wengine. Kama ambavyo nimetoa wito kwa taasisi na wadau wengine kuiga kwa NMB, Nitumie fursa hii pia kuziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa – ambazo ni Taasisi ya Serikali, lichukueni hili kama ajenda.

“Hakikisheni watoto hawa walemavu, yatima, wanaoishi mazingira magumu na wenye mahitaji maalum, wasiwe wanafikiwa tu kipindi cha Ramadhani, iwe ni utaratibu wa kila siku katika maisha yao yote,” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, katika Iftar ya mjini Unguja, alisema SMZ inaipongeza NMB kwa kudumisha utamaduni chanya wa kufuturisha wateja, sambamba na kusaidia watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu visiwani humo, ikiwemo kuwaalika futari.

“Tunaishukuru Menejimenti ya NMB kwa kulifanya tukio hili kuwa endelevu, lakini mwaka huu mkaenda mbele zaidi kwa kutenga fungu la kununulia na kukabidhi misaada hii muhimu kwa watoto. Hakika mnastahili pongezi.

“Watoto hawa mnaowasaidia leo na wateja waliohudhuria Iftar hii na hata wale ambao hawakupata fursa hiyo, wataendelea kuheshimu na kuthamini huduma zenu,” alisema Makamu wa Pili wa Rais.

Wakati wa Iftar iliyojumuisha watoto yatima wa Vituo vya Zamzam na Darul Maarifu vya jijini Dodoma, Spika, Dk. Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, alisema NMB imefanya ibada kubwa kuwashika mkono watoto hao katika kipindi cha Ramadhan.

“Ni matumaini yetu kuwa kwa kazi nzuri mnayofanya NMB, ikiwemo kujali na kuthamini haya makundi maalum, mafanikio yenu yatakuwa makubwa zaidi na miaka ijayo tutashuhudia hafla hizi mikoani, kwa sababu Allah atakuongezeeni kutokana na ibada zenu za kujali wenye uhitaji,” alimaliza.

NENO LA WANUFAIKA

Darul Maarifa – Masjid Gaddafi, Airport Dodoma: “Kwa niaba ya uongozi na wanafunzi wote wa Darul Maarifa, tumefurahia mwaliko wa Iftar, lakini zaidi misaada ya kijamii kwa ajili ya Ramadhani na Sikukuu ya Eid el Fitri. Wadau wavisapoti vituo hivi kote nchini, kwani vina changamoto nyingi,” Ustaadh Awamu Hamimu – Mwanafunzi Kiongozi Darul Maarifa.

Mazizini Orphanage Center – Zanzibar: “Hiki kilichofanywa na NMB kinapaswa kukimbiliwa na kila mmoja, ni ibada kubwa sana. Changamoto katika vituo hivi ni nyingi mno, kwahiyo tunaziomba taasisi zingine na wadau mmoja mmoja kufuata nyayo za NMB, tena wasisubiri tu kipindi cha Ramadhani, iwe kila siku,” Mwalimu Hassan – Kiongozi Mazizini Center.

Zamzam Islamic School – Mihuji, Dodoma; “Tunatoa shukrani za dhati kwa mwaliko huu wa Iftar iliyoandaliwa na NMB, lakini pia kwa misaada tuliyopewa hapa. Tunawaombea NMB mafanikio ili kusaidia vituo vingi zaidi vya mayatima. Wadau zaidi wajitokeze kutusaidia,” Ustaadh Hamid Nassor Salum, Mlezi Zamzam Islamic.

Kidundo Orphanage Center – Zanzibar: “Kituo chetu kinajumuisha watoto yatima, wanaoishi kwenye mazingira magumu na wazee wasiojiweza, baadhi yao tunaishi nao pamoja kituoni, lakini wengine tunawahudumia wakiwa kwao. Tunahitaji uwezeshaji kama huu wa NMB ili kumudu kuishi nao pamoja wote. Tunatamani kuona kila mdau anafanya kama hiki kilichofanywa na NMB,” Khalid Kidundo – Mwenyekiti Kidundo.

Al Zam Center (cha Mbagala Zakhiem, Dar), Umrah Center (Magomeni Mikumi, Dar) na Tanzania Kwanza Center (Kigamboni, Dar), nao kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya Dar es Salaam, walitoa shukrani za dhati kwa misaada waliyopewa na NMB mbele ya Waziri Mkuu na kutaka agizo la kiongozi huyo kwa Serikali za Mitaa, lifanyiwe kazi.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here