Home KITAIFA SERIKALI YATOA MILIONI 399/- KWA WANANCHI WALIOATHIRIWA NA TEMBO NACHINGWEA

SERIKALI YATOA MILIONI 399/- KWA WANANCHI WALIOATHIRIWA NA TEMBO NACHINGWEA

Google search engine
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu
Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja
Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni TAWA, Linus Chuwa

Na MWANDISHI WETU

-NACHINGWEA

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho na kifuta machozi  cha zaidi ya shillingi millioni 399 kwa  wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika Wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 9, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, ziara iliyofanywa na TAWA mkoani hapa.

“Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, wahanga zaidi ya 1658 kwenye wilaya ya Nachingwea walipatikana lakini fedha ambazo Dk. Samia Suluhu Hassan kazileta kwa ajili ya kifuta jasho mwaka jana ni Shilingi milioni  399.4  na wale wote ambao waliokuwa wanastahili kupata kifuta jasho waliweza kukipata kifuta jasho hicho,” amesem DC Moyo

Amesema wilaya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu hususani tembo wanaoathiri mali na maisha ya wananchi  lakini pamoja na changamoto hizo amekiri  kuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA na TAWIRI katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.

“Jitihada za TAWA zimefanyika mara nyingi na mimi mwenyewe nimekuwa nikishiriki, jitihada moja ni kwa kutumia helikopta katika kuwaswaga au kuwafukuza wanyama tembo,” amesema

Akibainisha jitihada zilizofanywa na TAWA Katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu Kanda ya Kusini Mashariki, Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni Linus Chuwa amesema TAWA imeanzisha vituo 10 vya Askari wa kukabiliana na wanyamapori hao ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu  na vingine  vitano ni vya muda mfupi hasa pale matukio ya wanyamapori hao yanapojitokeza.

TAWA pia imefanikiwa kununua gari jipya katika kituo cha malola ambalo hutumiwa na Askari wa kituo hicho, pia imenunua ndege nyuki (drones) maalumu kwa ajili ya kufukuzia tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kufukuza tembo 2023, zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Jitihada zingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni  viongozi wa makundi  na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu.

Mhifadhi Mkuu Linus Chuwa ameongeza kusema  TAWA  imepeleka Askari wa wanyamapori wa vijiji 41 (VGS)  katika chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu na amethibitisha kuwa Askari hao hutumiwa na TAWA Katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori hao

Kwa upande wake, Afisa habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo Mkoani humo ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA Katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kuwahakikishia wananchi kuwa TAWA iko kazini kuhakikisha inafanya Kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama vile TAWIRI, GIZ na TANAPA.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here