Na MWANDISHI WETU
-MSALALA, KAHAMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Msalala, Khamis Katimba amesema, halmashauri hiyo inatarajia kuvuka lengo la ukusanyaji mapato kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.
Amesema, katika kipindi cha miezi tisa, halmashauri hiyo imefanikiwa kukusanya mapato kwa asilimia 91 Shilingi Bilioni 4.6 ya lengo Shilingi Bilioni 5.
Na kwamba, katika kipindi kilichobaki amesema, halmashauri hiyo inatarajio kukamilisha pia kuvuka lengo kwa makusanyo ya milioni 500 zaidi.
Katimba amesema, ni kutokana na ushirikiano wa watumishi wa halmashauri hiyo na mikakati iliyowekwa.
Alitoa kauli hiyo wakati wa ufunguzi wa stendi mpya ya Isaka ambapo alisema, miradi mbalimbali iliyopo kwenye halmashauri hiyo, ndio vyanzo vikuu vya mapato ya serikali.
“Katika miezi tisa pekee tumefanikiwa kufikisha asilimia 91 (Bil 4.6) ya mapato, hii maana yake tunao uwezo wa kuvuka lengo letu la kukusanya Bil 5 kwa miezi 12,” amesema.
Akizungumzia ujenzi wa stendi mpya ya mabasi Isaka, Katimba amesema stendi hiyo itaongeza wigo wa uchumi kwa wananchi pamoja na mapato ya halmashauri hiyo.
“Serikali inajitahidi kutekeleza malengo yake kama ilivyoahidi hivyo, wananchi nao wajitahidi katika ulipaji tozo na kodi mbalimbali za serikali.
“Serikali ni ya wananchi, tunapaswa kulipa tozo mbalimbali za serikali na kujiepusha na utoroshaji au ukwepaji wa kulipa kodi kwa kuwa, fedha zinazokusanywa hutumika kwa shughuli za maendeleo ya jamii ikiwemo ujenzi huu wa tendi,” amesema Katimba.
Kwenye ufunguzi huo, mkurugenzi huyo amesema, stendi ya Isaka ni moja ya mipango ya muda mrefu ya serikali na kwamba, ufunguzi wake utaeleta afueni pia utaongeza wigo wa uchumi kwa wananchi na serikali.
“Natoa wito kwa wananchi wa Halmashauri ya Msalala na maeneo jirani kuitumia stendi hii kwani uwepo wake ni moja ya sababu za ukuaji wa mji wa Isaka.
“Pia changamkieni viwanja kwani halmashauri imevipima karibu na stendi pembezoni mwa Barabara ya Isaka – Rwanda,” amesema.
Mkurugenzi huyo amesema, pamoja na mambo mengine, stendi hiyo imelenga kutoa huduma ya usafiri na usafirishaji pia halmashauri hiyo kuongeza kipato kwa ajili ya kuhudumia wananchi kwani ni chanzo cha uhakika.
Aliahidi kuwa, yeye na timu yake ya wataalam wataendelea na jitihada za kuhakikisha mapato yanakusanywa na kutumika kama inavyoelekezwa na serikali.
Pia alisema, hadi kufika Machi 31, 2024 halmashauri hiyo tayari imekusanya asilimia 91 ya makusanyo ya Mfuko Mkuu ambayo ni sawa na Shilingi Bilioni 4.6.
Ofisa Mapato wa Halmashauri hiyo, Salehe Msosole alishukuru uongozi wa halmashauri kwa kuweka msisitizo utendaji uliotukuka kwa watumishi wake ambao umesaidia kuongeza mapato ya halmashauri.
“Ukweli ulio wazi ni kuwa, ushirikiano wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Mibako Mabubu na mkurugenzi wetu (Katimba) pamoja na watumishi umesaidia sana halmashauri hii.
“…hasa kuweka kipaumbele cha kwanza katika utendaji kazi wa kila siku, jambo ambalo limesababisha usimamizi mzuri wa mapato hasa msisitizo wa kila diwani katika eneo lake huhakikisha tozo za serikali zinalipwa kama inavyotakiwa,” amesema Msosole.
Ofisa mapato huyo alisema, mkurugenzi wa halmashauri hiyo aliunde kikosi kazi ambacho anakisimamia.
“Mimi nasimamia kikosi hicho, tunafanya doria usiku na mchana kuhakikisha tunadhibiti utoroshaji wa mapato, tangu tuanze usimamizi huu kila siku tunakamata magari yasiyopungua manne na Bajaj mbili.
“Natoa wito kwa wafanyabiashara kulipa tozo za halmashauri kwa hiari ili kujenga uchumi wa nchi yetu na kumuunga mkono Rais wetu Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mgeni rasmi katika ufunguzi wa stendi hiyo, Majuto Pazi ambaye ni Diwani wa Kata ya Isaka aliwaomba wananchi hasa wana Isaka kutumia fursa ya stemndi hiyo hiyo kujiongezea kipato.
Ofisa Mipango wa halamahauri hiyoi, amesema kukamilika kwa stendi hiyo, ni jitihada za pamoja za mkurugenzi mtendaji, madiwani, wataalam wa halmashauri ngazi za vijiji, kata, wenyeviti wa vijiji na wananchi wote.
“Namshukuru Rais Samia kwa kuleta fedha za kuwezesha kujenga stendi hii sambamba na Mbunge wa Jimbo la Msalala, Idd Kassim Idd kwa ushawishi, kusimamia na kuhakikisha serikali na wawekezaji wanatoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ndani ya halmashauri.
Wananchi wanaozunguka stendi hiyo wameeleza kufurahishwa kwao na ufunguzi huo kwani, uongozi wa kijiji umetangaza kugawa maeneo ya biashara ndani ya stendi hiyo.