Home KITAIFA KIMBUNGA HIDAYA CHALETA MTIKISIKO NCHINI

KIMBUNGA HIDAYA CHALETA MTIKISIKO NCHINI

Google search engine

*CHAFIKIA ENEO LA BAHARI TAKRIBAN KILOMITA 125 KUTOKA PWANI YA KILWA, MVUA YATIKISA KIASI CHA MILIMITA 111.3 KWA KIPINDI CHA SAA SITA MFULULIZO

*UPEPO MKALI WATAWALA MAENEO YA PWANI DAR, UMEME WAKATI KWA SAA KADHAA

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kutoa taarifa ya mwenendo wa Kimbunga Hidaya  kilichopo karibu na maeneo ya Pwani ya nchi.

Taarifa ya TMA ilieleza kuwa hadi kufikia saa 9 usiku wa kuamkia leo, Kimbunga Hidaya  kilikuwa katika eneo la bahari takriban kilomita 125 kutoka Pwani ya Kilwa (Mkoa wa Lindi), kilomita 93 kutoka Pwani ya Mafia na kilomita 128 kutoka Pwani ya Dar es salaam kikiwa na mgandamizo wa hewa wa kiasi cha 985 na kasi ya upepo unaofika kilomita 120 kwa saa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa tangu usiku wa kuamkia wa leo, matukio ya upepo mkali na mvua kubwa zinazosababishwa na uwepo wa kimbunga hicho yameendelea kujitokeza ambapo hadi kufika saa 3 asubuhi, kituo cha hali ya hewa cha Kilwa Masoko (Lindi) kimeripoti mvua ya jumla ya kiasi cha milimita 111.3 kwa kipindi cha saa sita.

Kiwango hicho cha mvua kinatajwa kuwa ni kikubwa ukizingatia kuwa wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko ni milimita 96.6 tu.

“Hivyo kiasi cha mvua kilichonyesha ndani ya masaa 24 katika kituo cha Kilwa Masoko ni takribani asilimia 115 ya wastani wa mvua kwa mwezi Mei kwa kituo cha Kilwa Masoko.

“Viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine katika kipindi hicho ni milimita 90.7 kwa Mtwara na milimita 85.3 katika kituo cha hali ya hewa Naliendele (Mtwara),” ilieleza taarifa hiyo ya TMA

Kwa mujibu wa TMA, Kimbunga Hidaya kinatarajiwa kuendelea kusogea karibu zaidi na ukanda wa pwani ya nchi huku kikipungua nguvu taratibu kuelekea usiku wa kuamkia Jumapili Mei 5, 2024.

UMEME WAKATI SAA KADHAA

Hata hivyo kutokana na hekaheka ya Kimbnga Hidaya, Sehemu kubwa ya nchini ilikosa umeme usiku wa kuamkia Jumamosi wakati mvua kubwa na upepo mkali wa Kimbunga Hidaya kikikaribia kuipiga nchi hiyo ya Afrika Mashariki kufuatia wiki kadhaa za mafuriko kwenye ukanda huo.

Shirika la umeme la Tanzania (TANESCO), lilitangaza kukatika kwa umeme kulitokana na hitilafu ya gridi ya Taifa.

Taarifa hiyo ilitolewa jana kabla ya kukaribia Kimbunga Hidaya, ambapo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ilisema kuwa kimbunga hicho kilikuwa kinaelekea Pwani ya Tanzania.

Huduma za usafiri wa maboti baina ya mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam, na visiwa vya Zanzibar ulisitishwa wakati Kimbunga Hidaya kikikaribia pwani ya Afrika Mashariki kikiwa na kasi ya kilomita 120 kwa saa na huku kukiwa na upepo mkali.

Serikali ilionya kwamba wananchi wanapaswa kuchukuwa hadhari kubwa wakati huu kimbunga kikikaribia.

Usiku wa kuamkia jana (Jumamosi), mvua kubwa zaidi kuliko ya kawaida iliripotiwa kunyesha kwenye maeneo hayo, na mamlaka za nchi hiyo zilisema huenda hali ikaendelea kubakia hivyo hadi siku ya Jumanne (Mei 7).

Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania (Red Cross), limekuwa ikifanya kampeni za kuwaandaa watu na kile kinachoweza kujiri kwenye maeneo ya Pwani.

KASI YA KIMBUNGA HIDAYA

Kimbunga hicho, ambacho kinatembea kwenye eneo la magharibi ya Bahari ya Hindi kinatazamiwa kupita Dar es Salaam jioni ya Jumamosi au alfajiri ya Jumapili, lakini hakitarajiwi kukaa hapo kwa muda mrefu, kwa mujibu wa taasisi ya kufuatilia vimbunga, Global Disaster Alert and Coordination System (GDACS).

Kwa mujibu wa Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), mvua na mafuriko makubwa yaliyoanza tangu mwezi Machi yamesababisha maafa makubwa katika mataifa ya Tanzania, Burundi, Kenya, Somalia, Rwanda na sehemu nyengine za Afrika Mashariki.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here