Home MICHEZO NMB YAKABIDHI VIFAA VYA MILIONI 16.7/- TIMU ZA MAJESHI TANZANIA

NMB YAKABIDHI VIFAA VYA MILIONI 16.7/- TIMU ZA MAJESHI TANZANIA

Google search engine
Mkuu wa Idara ya wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Aikansia Muro akimkabidhi vifaa vya Michezo Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania, Kanali Robert Mbuba kwa ajili ya michezo inayotarajia kufanyika Julai na Agosti mwaka huu. Kushoto ni Kamishana msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto na uokoaji, Laizer Loshipay na kulia ni Meneja Mwandamizi wa mauzo idara  ya Biashara NMB, Isaac Mgwassa na Meneja Mwandamizi wa Idara ya wateja Binafsi, Ally Ngingite.

Na MWANDISHI WETU

-DAR E S SALAAM

BENKI ya NMB imekabidhi vifaa vya michezo vyenye thamani ya Shilingi milioni 16.7,  ambavyo ni sehemu ya udhamini kwa timu zitakazoshiriki Mashindano ya Baraza la Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA), itakayofanyika Julai mwaka huu mjini Morogoro.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na jezi za mpira wa miguu 154, jezi za mpira wa kikapu pea 84, ‘tracksuit’ 32 na fulana ‘t-shirt’ 250, zitakazovaliwa na timu za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi, Zimamoto, Jeshi la Wananchi (JWTZ), Uhamiaji, Magereza na Idara Maalum za SMZ.

Mkuu wa Idara ya Wateja Binafsi wa NMB, Aikansia Muro, ndiye aliyekabidhi vifaa hivyo leo jijini Dar es Salaam kwa Kanali Robert Mbuba, aliyepokea kwa niaba ya Mwenyekiti wa BAMMATA, Brigedia General Saidi.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Zimamoto na Uokoaji, Laizer Loshipay, Aikansia aliipongeza Kamati ya Mashindano ya BAMMATA kwa kuratibu na kusimamia michezo hiyo muhimu kwa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

“Tunajisikia furaha kwa mara nyingine tena kuwa sehemu ya mashindano haya na tumekutana hapa kukabidhi vifaa mbalimbali ambavyo ni sehemu ya udhamini wetu kwa timu za majeshi yetu Tanzania Bara na Visiwani yanayoshiriki BAMMATA 2024.

“Kwa takribani miaka minne sasa, NMB tumekuwa tukidhamini michezo hii inayoratibiwa na BAMMATA na tunaamini ushirikiano huu wa muda mrefu utaendelea kuwa na manufaa kwa pande zote mbili kwa maana na NMB na Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

“Kwa kutambua umuhimu wa michezo kwenye jamii na kwa kuthamini maudhuhi yanayobebwa na mashindano haya, tumeamua kutoa udhamini wa Shilingi milioni 16.7 kwa ajili ya kufanikisha mashindano ya mwaka huu mjini Morogoro,” alisema Aikansia.

Alibainisha kuwa NMB imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali nchini, ambako kwa nyakati tofauti wamedhamini Taifa Stars, Azam FC, timu za mpira wa magongo pamoja, Kombe la Mkuu wa Majeshi la Gofu ‘CDF Trophy’ na mashirikiano na klabu za Simba na Yanga.

Kwa upande wake, Kanali Mbuba kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya BAMMATA, aliishukuru NMB kwa udhamini wao unaoenda kufanikisha mashindano hayo ya timu za Majeshi ambazo zitatumia vifaa hivyo kama chachu ya kufanya vizuri.

“BAMMATA tumefurahishwa na tukio hili, na ahadi yetu kwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya NMB ni kwamba tutaendelea kuwa wateja wa benki hii, ambayo imekuwa na huduma bora na rafiki kwetu na kwa jamii kwa ujumla.

“Kwa niaba ya Mwenyekiti wa BAMMATA, Brigedia General Saidi, tunaomba mashirikiano haya yawe endelevu na matarajio yetu ni kuona siku moja NMB inaingia mkataba wa kuwa Mdhamini Mkuu wa mashindano haya kwa miaka ijayo,” alisema Kanali Mbuba.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here