Home KITAIFA HATIFUNGANI YA NMB JAMII YAANZA KUUZWA SOKO LA HISA LONDON

HATIFUNGANI YA NMB JAMII YAANZA KUUZWA SOKO LA HISA LONDON

Google search engine

Na MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB imetanua wigo wa kushiriki katika masoko ya mitaji kimataifa kwa kuiorodhesha hatifungani yake ya jamii (NMB Jamii Bond) jana katika Soko la Hisa la London (LSE).

Hatua hiyo inaifanya NMB kuwa taasisi ya kwanza Tanzania kuwa na hatifungani katika soko hilo kubwa kuliko yote ya hisa duniani na benki ya kwanza Afrika Mashariki, Kati na Kusini kuorodhesha hatifungani ya uendelevu LSE.

Kuorodheshwa kwa mara ya pili kwa NMB Jamii Bond katika masoko ya hisa ya nje kunafuatia kuidhinishwa kwake mwezi jana kuuzwa katika Soko la Hisa la Luxembourg ambako pia hatifungani ya NMB Jasiri Gender Bond imekuwa ikifanya vizuri tangu iorodheshwe kwenye soko hilo mwaka jana.

Uzinduzi wa mauzo ya Hatifungani ya Jamii ulifanyika wakati wa ufunguzi wa shughuli za wiki hii za LSE, maarufu duniani kwa kuendeleza uwekezaji unaozingatia masuala ya mabadiliko ya tabia, ufadhili wa uendelevu na uwekezaji wa kijani.

Afisa Mtendaji Mkuu wake, Julia Hoggett, alisema LSE inajivunia kuhusishwa na dhamana hiyo anzilishi ya ufadhili wa uendelevu ya NMB ambayo ni ubunifu mahususi kwa ajili ya kuchochea uwekezaji katika miradi yenye tija kijamii na kimazingira.

“Mtaji unaotokana na uorodheshwaji huu in dola milioni 73 na unaendana na jitihada za kimataifa za kukabiliana na changamoto za uendelevu ili kuwa na jamii thabiti na endelevu,” Hoggett alibainisha katika hotuba yake.

Aidha, alisema hatifungani hiyo kubwa ya uendelevu kuwahi kutolewa katika ukanda huu pia ni fursa kwa wawekezaji kutengeneza faida huku wakichangia kuboresha maisha na  kusaidia kuilinda asili ya dunia.

Benki ya NMB iliiweka sokoni NMB Jamii Bond mwaka jana kupata Shilingi bilioni 75 za Kitanzania na dola za Kimarekani milioni 10 kukiwepo na fursa ya kuongeza Shilingi bilioni 25 na dola milioni 5.

Ikithibitisha ukopeshekaji wa benki hiyo na kuonesha utayari wa wawekezaji kuunga mkono ajenda ya uendelevu ya taasisi hiyo, mauzo ya Hatifungani ya Jamii yalizidi kwa asilimia 284 upande wa shilingi na dola asilimia 730 nakupelekea kupatikana jumla ya TZS bilioni 400 (takribani dola milioni 160).

Afisa Mtendaji Mkuu Ruth Zaipuna aliyewaongoza maafisa wa NMB kushuhudia tukio hilo alisema uorodheshwaji huo wa kihistoria unaiweka pazuri benki hiyo katika masoko ya fedha duniani na kwenye macho ya jumuiya ya wawekezaji wa kimataifa.

“Kuorodheshwa leo kwa Hatifungani ya Jamii kunaimarisha nafasi ya Benki ya NMB kama mwanzilishi wa uendelevu katika soko la mitaji Afrika na sasa katika hatua hii ya kimataifa,”  alisema Zaipuna aliyezidiwa na furaha ya maendeleo hayo.

Miongoni mwa waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza, Mbelwa Kairuki na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo wa Uingereza, Andrew Mitchell, ambao uwepo wao ulionesha kuwa kuiorodhesha hatifungani hiyo pia ni jambo jema kidiplomasia.

“Mafanikio haya kipekee yanadhihirisha imani waliyokuwa nayo wawekezaji wa Kitanzania na kimataifa katika uthabiti wa Benki ya NMB na dhamira yake ya uendelevu katika utendaji wake, biashara, jamii na masuala ya mazingira,” alisema Zaipuna

NMB ilianza kuziingiza hatifungani zake katika masoko ya kimataifa mwaka 2022 ikianza na NMB Jasiri Bond, dhamana inayolenga hasa kuwafadhili  wanawake wajasiriamali na wanaomiliki biashara, ambayo mauzo yake ya asilimia 197 yameifanya kushinda tuzo kadhaa za kimatifa.

Zaipuna alisema masoko ya kimataifa yanaiwezesha benki hiyo kuwa na wigo mpana wa kupata fedha kwa ajili ya kufadhili miradi inayosaidia kuboresha maisha, kubadilisha jamii na kuwa na mustakabali bora kwa watu wote.

Jamii Bond ni toleo la kwanza la Waraka wa Matarajio wa Benki ya NMB wa Programu ya Utoaji wa Hatifungani ya Muda wa Kati wa sasa hivi wa miaka 10 wenye thamani ya Shilingi trillion 1 ambao mapato yake yatatumika kufadhili miradi yenye tija kama nishati mbadala, usalama wa chakula, majengo ya kijani, na kutengeneza ajira.

“Tulianza kwa kuiorodhesha hatifungani hii katika Soko la Hisa la Luxembourg mwezi uliopita, na leo tunaiorodhesha hapa LSE ili kuwapa wawekezaji wanaozingatia uendelevu, fursa ya kuchangia mabadiliko huku wakipata faida nzuri ya uwekezaji wao,” alisema Zaipuna

Alisema NMB ambayo mtaji wake wa soko wa USD bilioni 1 kunaifanya kuwa benki ya pili kubwa iliyoorodheshwa Afrika Mashariki, itaendeleza nia yake ya dhati ya kuchagiza maendeleo endelevu na kuhakikisha umakini katika uwekezaji.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo aliongeza kuwa NMB Jamii Bond ni matokeo ya benki hiyo kuzingatia umuhimu wa fedha na ufadhili katika kuleta maendeleo endelevu na kuchangia kutatua changamoto zinazozikabili jamii na sayari yetu.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here