Na MWANDISHI WETU
-IRINGA
SERIKALI imetoa tahadhari dhidi ya dawa zinazotembezwa mkononi ikiwa ni pamoja na zinazouzwa katika vyombo vya usafiri kinyume na sheria ikitaja dawa nyingi ni duni na bandia.
Hayo yamesemwa leo Mei 16, 2024, mjini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba kwenye ufunguzi wa kikao kazi kati ya wahariri wa habari kutoka vyombo mbalimbali na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
“Wananchi waache mara moja kununua dawa zinazotembezwa mikononi ikiwa ni pamoja na katika vyombo vya usafiri kinyume cha sheria kwani mara zote dawa hizo huwa ni duni au bandia.
“Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote atakayepatikana na dawa bandia kwa kigezo kuwa hawakujua kwamba ni bandia wakati huo huo akiwa amesababisha madhara kwa wagonjwa,”alisema
RC Serukamba, alisema kuwa Dawa na Vifaa Tiba ni bidhaa nyeti na zenye madhara makubwa na kwamba ikiwa havikudhibitiwa ipasavyo zinaweza kusababisha ulemavu na kupoteza maisha, hivyo kudhoofisha uchumi wa nchi.
“TMDA ina ina jukumu la msingi katika kuhakikisha afya ya wananchi inalindwa na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha bidhaa zilizopo katika soko ni salama na zenye ubora,” amesema Serukamba.
Aidha, katika kukabiliana na changamoto hiyo, amewasihi Wahariri wa Habari kuendelea kushirikiana na TMDA kupitia matumizi ya kalamu na zao kutoa elimu kwa jamii kwani kwa kufanya hivyo jamii itaweza kuifahamu taasisi hiyo na kazi zake hivyo kuweza kutoa taarifa pale wanapotilia mashaka ya ubora na usalama wa bidhaa za Dawa na Vifaa Tiba zilizopo sokoni ili hatua stahiki zichukuliwe.
Akizungumzia uwepo wa matangazo ya Dawa kichume cha sheria, amesema Mamlaka hiyo ina jukumu la kudhibiti matangazo ya bidhaa hiyo ili kuzuia matangazo yenye nia yaekupotosha umma kwa lengo la Kibiashara.
“Napenda kuwaeleza kuwa suala la kudhibiti matangazo ni la Kisheria na katika kutekeleza Utekelezaji wake, zipo Kanuni za Udhibiti Matangazo ya Dawa na Vifaa tiba zilizoandaliwa chini ya Sheria Sura 219 zilizoanza kutumika mwaka 2010,” amesema