Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama kuwa mwaka 2023 umekuwa wa kipekee katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwani tumefanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mapambano ya dawa za kulevya hapa nchini.
Amesema Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 1,965,340.52 zikihusisha watuhumiwa 10,522 (wanaume 9,701 na wanawake 821).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 16, 2024 Jijini Dodoma, Waziri Jenista alisema kuwa Dawa za kulevya zilizokamatwa ni Heroin Kilogramu 1,314.28, Cocaine kilogramu 3.04, Methamphetamine 2 Kilogramu 2,410.82, Bangi Kilogramu 1,758,453.58, Mirungi Kilogramu 202,737.51, Skanka Kilogramu 423.54 na Dawa Tiba zenye Asili ya Kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672.
Aidha, amesema kiasi hicho cha dawa za kulevya kilogramu1,965,340.52 zilizokamatwa katika kipindi cha Januari – Desemba 2023, ni karibu mara tatu ya kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa nchini kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilogramu 660,465.4.
“Aidha, dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi pia zilikamatwa katika kipindi hicho.
“Katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanaimarishwa nchini, Serikali imenunu Boti yenye mwendo kasi (Speed Boat) ambayo pamoja na shughuli zingine itakuwa ikifanya doria baharini ili kufuatilia vyombo vinavyohisiwa kuingiza dawa za kulevya nchini kama vile Heroini, Methamphetamine na nyingine.
“Boti hii ilizinduliwa rasmi tarehe 28 April, 2024 Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa .Uwekezaji huu mkubwa juu ya vita dhidi ya dawa za kulevya na ukamataji mkubwa uliofanyika mwaka 2023, unadhihirisha dhamira ya dhati na utashi wa kisiasa wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan,” amesema
Pamoja na hali hiyo amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo. Hadi kufika Desemba 2023, Serikali ilikuwa na vituo 16 vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics). Vituo hivi viliwahudumia waraibu wa dawa za kulevya 15,912.
“Aidha, katika kipindi hicho kulikuwa na nyumba 56 za upataji nafuu (sober houses) zikihudumia waraibu 3,488. Serikali ilisimamia kikamilifu uanzishaji na Uendeshaji wa nyumba hizi. Pia, tiba ya uraibu wa dawa za kulevya hutolewa kwenye vitengo vya afya ya akili vilivyopo katika Hospitali za Wilaya, Mikoa na rufaa nchini. Hadi kufikia mwezi Desemba mwaka 2023, jumla ya waraibu 903,062 wa dawa za kulevya na vilevi vingine walipatiwa huduma katika hospitali hizo.
“Hii ni hatua muhimu katika kupunguza madhara yanayotokana na matumizi ya dawa za kulevya kama vile, Uraibu, UKIMWI, Kifua Kikuu, Homa ya ini, Magonjwa ya akili na magonjwa mengine yasiyoambukiza. Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Taifa cha Utengamao (National Rehabilitation Centre) kwa ajili ya kuwahudumia waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu.
“Hatua za mwanzo za ujenzi wa kituo hiki kinachojengwa katika eneo la Itega Jijini Dodoma zimeshaanza. Ujenzi wa kituo hiki utasaidia kuwajengea uwezo waraibu wa dawa za kulevya waliopata nafuu ili waweze kujikimu kimaisha na hivyo kutokurejea kwenye matumizi ya dawa za kulevya. Katika kuzuia matumizi ya dawa za kulevya nchini, Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya pamoja na wadau wengine, iliendelea kutoa elimu juu ya madhara ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya katika jamii ili jamii isijiingize kwenye matumizi ya dawa hizo,” amesema