Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amevihimiza vyombo vya Habari, kutokubali kutumika na Baadhi ya Wanasiasa wenye dhamira ya kutaka kuligawa taifa, hasa kipindi hiki ambacho Taifa linajiandaa kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi mkuu wa 2025.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo Juni 18, 2024 jijini Dar e es Salaam, wakati akifungua Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya habari nchini.
“Kuelekea Chaguzi zinazokuja msikubali kuingia kwenye mtego wa kulirarua taifa, toeni taarifa kwa haki na kwa kuzingatia weledi wa taaluma yenu, toeni taarifa za Rushwa kwenye Uchaguzi,” amesema Rais Samia.
SUNGURA NA SERA YA UWEKEZAJI
Awali akizungumza mbele ya Rais Samia, Mwenyekiti wa wanaopigania haki ya kupata taarifa ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT) Ernest Sungura amemuomba Rais Dk. Samia kuangalia namna ya kubadili sera ya uwekezaji kwenye tasnia ya habari hasa kwa wageni.
Kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 mwekezaji mgeni katika sekta ya habari hatakiwi kuwa na hisa zinazozidi asilimia 49 jambo linaloelezwa kukwamisha ukuaji wa uchumi wa wanahabari na sekta ya habari kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo, Tido Mhando ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya kutathmini uchumi wa vyombo vya habari amependekeza uwekezaji kwa wageni ufikie asilimia 75 katika maboresho ya sheria yanayotazamiwa siku za usoni.
Katika hatua nyingine Sungura ameeleza kuwa bado kuna changamoto ya waandishi wa habari kufanya kazi pasina mikataba, ujira mdogo na wakati mwingine mishahara yao kuchelewa.
Amesema kuwa kanuni za ajira zinaelekeza mambo mengi kuhusu masuala ya ajira ikiwamo kuwa na mikataba ya kudumu na kama mikataba ni ya muda basi isipungue miezi 12 hivyo ameomba utiliwaji mkazo wa sheria hizo kuwasaidia wanahabari kupata haki zao ikiwamo Bima ya Afya, michango ya NSSF na fidia.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya habari na Tanzania imekuwa kinara Afrika Mashariki kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kutokana na Rais Samia kuwataka wakuu wa mikoa na wilaya kuacha ubabe yeye alishaacha siku nyingi.
Pia alimshukuru Rais kwa namna anavyoendelea kupambana na ujenzi wa miundombinu hasa ya barabara katika mkoa wake ili Dar es Salaam iweze kuonekana bora zaidi.