Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema vyombo vya habari si mshindani wa Serikali bali ni mdau na mshiriki mzuri wa masuala ya sekta ya umma.
Amesema siku za nyuma vyombo vya habari vilikuwa katika mvutano na Serikali na hapakuonekana palipofikiwa.
Rais Samia ameyasema hayo leo Juni 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika kongamano la sekta ya habari linalofanyika jijini hapa.
“Katika kipindi hicho na mimi sina tafsiri ya kipindi hicho kama ninyi mlivyoandika kipindi hiki na mimi nasema kipindi hicho sina tafsiri,” amesema na kuibua furaha kutoka kwa wahudhuriaji.
Mkuu huyo wa nchi amesema kuwa uamuzi wa kukaa pamoja na vyombo vya habari na kuzungumza navyo, kadhalika kushirikiana navyo umeondoa mivutano.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira mazuri ya sekta ya habari, akirejea juhudi mbalimbali zinazofanywa kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya taaluma ya habari.
Amesema vyombo vya habari si adui wa serikali bali ni mdau muhimu, hivyo Serikali haina budi kuweka sera nzuri na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari.
Rais Samia amesema vyombo vya habari vikiwa huru vinagusa kila pembe ya jamii kwa kuelemisha, kufichua maovu , kuchangia maendeleo ya kijamii na kukuza demokrasia.
Amesema ni lazima waandishi wa watambua kwamba wana wajibu wa kuandika habari za kiuchambuzi kwenye vyombo vya habari kwani kwa sasa ni chache, hivyo waandishi watilie mkazo kwenye uchambuzi na wajielekeze kwenye habari zinazokubalika
Kutokana na hali hiyo amesema kuwa zama zinabadilika waandishi lazima waendane na mabadiliko yaliyopo ya kiteknolojia na watumie uwezo wao wa taaluma vizuri.
MAZINGIRA MAZURI
Rais Dkt. Samia pia aliahidi kuendelea kuweka mazingira mazuri kati ya wanahabari na serikali na kwamba eneo lililobakia ni dogo haswa haswa katika mabadiliko ya sera na baadhi ya sheria huku akiahidi kuendelea kulifanyia kazi.
“Dhahiri kwamba vyombo vya habari vinapitia mapinduzi ya utendaji kazi na kiutendaji hapa changamoto vyombo vya habari kushindwa kuendeana na kasi ya teknolojia iliyopoi, lazima waandishi wa habari wafanye kazi kwa bidii kujituma ili kuendana na kasi hiyo,” amesema
Alieleza kuwa changamoto ya mabadiliko makubwa ya teknolojia yanapaswa kuyakabili na sio kuyakimbia huku akieleza masikitiko yake kwenye mitandao ya kijamii inayopotosha taarifa .
“Kalamu zenu ni kali mno na jamii zetu zinapenda habari za ukakasi na kwamba ikitolewa habari yenye ukakasi na akitokea mtu akaifafanua atashambuliwa ,wanataka habari hizo hizo zenye ukakasi hivyo basi waandishi ni vyema kua makini ,” amesema