Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) inatekeleza Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo Mkubwa wa Kilovolti 400 wa Tanzania na Zambia (TAZA) kupitia Iringa ambao utasaidia kuboresha huduma ya upatikanaji wa umeme katika Mji wa Mafinga na maeneo jirani.
Kapinga amesema hayo Juni 18, 2024, Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mafinga, Kosato Chumi aliyetaka kufahamu Mpango wa Serikali wa kukabiliana na tatizo la umeme mdogo (Low Voltage) katika Mji wa Mafinga.
Amesema kupitia mradi huo, vitajengwa Vituo vya Kupokea na Kupoza Umeme katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Kisada kwa ajili ya kusambaza umeme katika mji wa Mafinga na maeneo jirani.
Mradi huo pia utaondoa tatizo la kuzidiwa uwezo katika njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa Kilomita 90 kutoka kituo cha Mafinga hadi Mgololo.