Home BIASHARA NMB YAPONGEZA  VYOMBO VYA HABARI KUSTAWISHA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA

NMB YAPONGEZA  VYOMBO VYA HABARI KUSTAWISHA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA

Google search engine
Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali Benki ya NMB Alfred Shayo, akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la pili la maendeleo ya sekta ya habari lililofanyika ukumbi wa Mlimani City,  Dar es Salaam leo Juni 18, 2024. Na Mpigapicha Wetu

Na MWANDISHI WETU

-DAR ES SALAAM

BENKI ya NMB imeipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mapinduzi chanya kwenye Sekta ya Habari Tanzania, huku ikikiri kuvutiwa na mchango wa vyombo vya habari katika kustawisha uchumi endelevu kupitia huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi.

Pongezi hizo zimetolewa leo Juni 18, 2024 jijini Dar es Salaam na Afisa Mkuu wa Wateja Wakubwa na Serikali wa NMB, Alfred Shao, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari na Kikao Kazi cha Maafisa Habari wa Serikali, lililofunguliwa na Rais Samia.

Kongamano hilo la siku mbili na Kikao Kazi cha siku nne, limefunguliwa Jumanne Juni 18, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, chini ya kaulimbiu; Jenga Mustakabali wa Endelevu Kwenye Sekta ya Habari Katika Zama za Kidijiti.’

Akizungumza katika kongamano hilo lililodhaminiwa na benki yake, Shao alisema Sekta ya Fedha, hasa NMB, inatambua na kuthamini mchango wa Serikali kupitia Wizara ya Habari na Teknolojia ya Habari na Vyombo vya Habari katika kuchochea Huduma Jumuishi kwa Wananchi.

“Mheshimiwa Rais, napenda kukupongeza wewe na Serikali yako kwa mapinduzi ya dhati katika sekta ya habari, hasa uhuru wa habari, ambao umeleta matokeo chanya sio tu katika habari, hata sekta nyingine ikiwemo ya fedha yaliyoleta ujumuishaji wananchi katika huduma za kifedha.

“Tunaipongeza Serikali kwa ongezeko kubwa la vyombo vya habari lililochangiwa na kuimarishwa kwa Sekta ya Habari, ongezeko linaloakisi uhuru wa habari ulioiwezesha Tanzania kutajwa kama kinara wa uhuru huo kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Kipekee kabisa Mheshimiwa Rais, naomba kumpongeza Waziri Nape Nnauye, wizara yake, waandishi na vyombo vyote vya habari kwa kazi kubwa ambayo wameifanya katika kuchochea kwa kiasi kikubwa ujumuishaji wananchi kwenye Sekta ya Fedha yaani ‘financial inclusion.’

“Wamefanya kazi kubwa kuelimisha wananchi kupitia Taasisi za Fedha, vilevile pale ambapo taasisi hizo zilikuja na masuluhisho yanayohusu wananchi, waandishi na vyombo vya habari wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha yanawafikia wananchi kwa lugha ambayo ni rahisi kuielewa.

“Kwa mfano, NMB mwaka huu tumekuja na Sera ya Huduma za Kibenki Vijijini (rural banking), ambayo tunaifanya kupitia mawakala, na magari yanayotembea (bank on wheel ), tukiwa na lengo la kutembelea vijiji vipatavyo 1,000 mwaka huu na kufungua akaunti milioni moja na nusu,” alisema Shayo

Kutokana na hali hiyo aliwashukuru wanahabari na vyombo vyao, kwa mchango wao wa kuifikisha sera hiyo vijijini, ambapo hadi hsasa NMB wamefika katika vijiji 500 na kufungua akaunti 700,000.

Alibainisha ya kwamba, NMB ni mdau mkubwa katika kukuza Uchumi Endelevu na wanaamini kwa kushirikiana na vyombo vya habari, wana uwezo mkubwa wao na taasisi zingine za fedha kuwafikia wananchi kwa uharaka, urahisi na wepesi na kuwajumuisha katika mnyororo huo.

“Uchumi endelevu unawezekana pale tu kunapokuwepo na Huduma Jumuishi za Kifedha kwa Wananchi na kwenye hili, tunaamini katika ushirikiano baina yetu na vyombo vya habari nchini.

“NMB imekuwa mdau mkubwa wa tasnia ya habari na vyombo vya habari na tumekuwa tukishirikiana navyo kwa miaka mingi, kwa sababu tunaamini ushirikiano wetu ni kwa manufaa ya wote na utasaidia kuleta Maendeleo Chanya kwa Wananchi wetu,” alisema Shayo.

Akitolea mfano wa ushirikiano wa NMB na vyombo vya habari, Shao alisema benki yake imekuwa mdhamini kwa miaka mitatu wa matukio yanayoihusisha Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), sambamba na udhamini wao kwa kongamano hilo linaloendelea jijini Dar es Salaam.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here