Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson ameelekeza Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kumhoji mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kwa madai ya utovu wa nidhamu.
Akitangaza uamuzi huo bungeni jijini Dodoma leo Jumanne, Juni 18, 2024 Dk Tulia amesema kuwa Mpina amedharau mamlaka ya Spika na Bunge kwa kufanya vitendo vya utovu wa nidhamu.
Awali, Mpina alipewa wiki moja kuwasilisha ushahidi wake baada ya kulieleza Bunge kuwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amelidanganya Bunge katika sakata la uagizaji wa sukari na badala yake ushahidi aliotakiwa kuuwalisha alikwenda kuueleza kwa vyombo vya habari kabla Spika wa Bunge hajatoa mwongozo wake kuhusu jambo hilo, ambapo kufanya hivyo ni kinyume na kanuni za Bunge.
Spika Ackson alitoa maelekezo haya bungeni jijini Dodoma, akieleza kuwa kitendo cha Mpina, ambaye ni Mbunge mzoefu anayejua kanuni za Bunge, kuwasilisha ushahidi wake na kisha kwenda kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu nyaraka hizo ni kitendo cha utovu wa nidhamu kwa Bunge na Spika Dk. Ackson aliongeza kuwa tabia hiyo ni kudharau mamlaka ya Spika na kuingilia mwenendo wa Bunge, hivyo kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, ushahidi unaowasilishwa kwa Spika haupaswi kujadiliwa nje ya Bunge mpaka utaratibu rasmi utakapo kamilika.
Kutokana na hali hiyo, Spika Dkt. Tulia alisisitiza kuwa kitendo cha Mpina ni cha kipekee katika kudharau taratibu za Bunge, jambo ambalo halikubaliki na linapaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu. Spika alionya kuwa kila Mbunge anapaswa kuheshimu taratibu na mamlaka za Bunge ili kudumisha nidhamu na heshima ndani ya chombo hicho muhimu cha uwakilishi wa wananchi.
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge inatarajiwa kumhoji Mpina na kutoa mapendekezo ya hatua zaidi za kinidhamu zinazopaswa kuchukuliwa dhidi yake.
Uchunguzi wa kamati hiyo utaangazia kama kitendo cha Mbunge Mpina kimevunja kanuni za Bunge na kudharau mamlaka ya Spika.
Hatua hiyo inakuja wakati ambapo Bunge linaendelea na vikao vyake vya kawaida, ambapo masuala mbalimbali ya kitaifa yanajadiliwa na kupitishwa kwa manufaa ya wananchi.
Dk. Tulia amesisitiza umuhimu wa wabunge kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa ili kudumisha nidhamu na heshima ya Bunge.
Spika pia aliongeza kuwa Bunge lina wajibu wa kulinda hadhi na heshima yake mbele ya wananchi wanaolitegemea kwa uwakilishi wa maslahi yao.
“Kitendo cha Mbunge Mpina kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu ushahidi aliouwasilisha ni mfano mbaya kwa wabunge wengine na kinaweza kuleta athari mbaya kwa mwenendo mzima wa Bunge,” amesema Dk. Tulia
Kwa sasa, wananchi na wadau mbalimbali wa siasa wanafuatilia kwa karibu hatua ambazo Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge itachukua dhidi ya Mbunge Mpina.
Ni matumaini ya wengi kuwa uamuzi utakaotolewa utakuwa wa haki na utakaosaidia kudumisha heshima na nidhamu ndani ya Bunge