Na MWANDISHI WETU
Rais Jamhuri ya Guinea Bissau, Umaro Sissoco Embaló anatarajia kufanya ziara ya siku tatu nchini yenye lengo la kukuza uhusiano na diplomasia kati ya Tanzania na Taifa hilo.
Ziara hiyo inatarajiwa kuanza kesho Juni 21 hadi Juni 23, 2024 ikilenga pia maeneo ya kushirikiana katika sekta mbalimbali za kimkakati ikiwemo uzalishaji wa zao la korosho na udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia Taasisi ya Muungano wa Viongozi wa Afrika katika Kudhibiti Malaria (ALMA).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Dkt. Samwel Shelukindo amesema kupitia ziara ya Rais Embaló, Tanzania na Guinea Bissau zimedhamiria kuimarisha na kuinua kiwango cha ufanyaji biashara na uwekezaji hasa kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
“Ziara hii hii itatoa fursa kwa nchi hizi mbili kujadili kwa kina namna ya kuendelea kupambana na kudhibiti ugonjwa hatari wa malaria, kwa kuzingatia Rais Embaló ni Mwenyekiti wa ALMA.
“ALMA ni taasisi ambayo ilianzishwa mwaka 2009 na viongozi wa nchi zote 55 za Afrika kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030,” amesema Balozi Shelukindo.