Home KITAIFA SERIKALI YAONDOA  HOFU UMEME  KUFIKA VITONGOJI VYOTE NCHINI

SERIKALI YAONDOA  HOFU UMEME  KUFIKA VITONGOJI VYOTE NCHINI

Google search engine

*NAIBU WAZIRI KAPINGA ATANGAZA KILA KONA KUNG’ARA KWA MWANGA WA UMEME, VITUO VYA KUPOZA UMEME KUJENGWA KILOSA, MBINGA NA HANANG’

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga

Na MWANDISHI WETU

-DODOMA

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata umeme ambapo mpaka sasa vitongoji  33,000 vimesambaziwa umeme kati ya vitongoji zaidi ya 60,000.

Hayo aliyasema leo Juni 21, 2024 Bungeni  Jijini Dodoma wakati akijibu maswali mbalimbali ya  wabunge katika kipindi cha Maswali na Majibu.

Kutokana na hali hiyo alisem kuwa kutokana na suala la maendeleo  kuwa ni  hatua,  Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.

 Akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Lupembe, Edwin Swale (CCM),  kuhusu mpango wa Serikali kupeleka umeme wa REA kwenye vitongoji,  ambapo Kapinga  alisema kuwa Jimbo la Lupembe lina vitongoji 227 ambapo vitongoji 118 vimekwishapatiwa umeme na vitongoji 109 vilivyobaki Serikali pia itavipelekea umeme.

Kutokana na hali hiyo aliongeza kuwa, vitongoji 19 kati ya hivyo vitapatiwa umeme kupitia mradi wa Ujazilizi Awamu ya Pili B ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu huku vitongoji 15 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Vitongoji 15 kila Jimbo, ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Aidha, alisema vitongoji  75 vitapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa “Hamlet Electrification Project” ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/25 kulingana na upatikanaji wa fedha.

Akizungumzia Kijiji cha Madeke na maeneo ya uwekezaji katika Mji wa Njombe kupatiwa umeme Naibu Waziri Kapinga, alisema kuwa Serikali itafuatilia ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Aliongeza kuwa, Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini mkubwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi.

Akijibu swali la Mbunge wa Manyoni Magharibi, Yahaya Masare (CCM), kuhusu kupeleka umeme kwenye vitongoji 15 vya Halmashauri ya Itigi,  alisema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa kuwapata Wakandarasi watakaotekeleza miradi hiyo, ikiwa ni  kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita.

Alisema kupitia  mwaka wa fedha unaokuja wa 2024/25, Serikali imetenga fedha za kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Minza Mjika,  wa Mkoa wa Simiyu aliyetaka kufahamu ni lini vitongoji ambavyo havina umeme katika  Mkoa wa Simiyu vitapata umeme, alisema ipo miradi inayoendelea kutekelezwa ukiwemo mradi wa ujazilizi na kuongeza kuwa,  kutokana na Serikali kuona umuhimu wa umeme kwa wananchi imebuni miradi mbalimbali itakayotimiza dhamira ya Serikali ya  kila mwananchi kupata huduma ya umeme.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya (Chadema), ambaye alitaka kufahamu kuhusu umeme kufika kwenye baadhi ya Kata ambazo zipo vijijini katika Jimbo la Bunda Mjini kati ya kata 14 kata saba zipo Vijijini, ambapo alisema kuwa kwa mwaka ujao wa fedha Serikali imefanya utaratibu wa kuhakikisha mitaa ya Bunda mjini ambayo haina umeme inapata umeme na itaendelea kupeleka umeme hadi kwenye vitongoji.

Aidha, akikibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Tunduru Kusini, Daimu Mpakate (CCM), kuhusu lini Mkandarasi anayetekeleza miradi ya ujazilizi ataanza kazi, Kapinga alisema kutokana na kuelekea kukamilika kwa miradi ya umeme vijijini, hivi karibuni inaanza miradi ya ujazilizi katika Vitongoji vya jimbo la Tunduru Kusini.

Aidha, kuhusiana na vijiji vingine kurukwa kupatiwa umeme aliwataka wabunge kutambua kuwa maendeleo ni hatua hivyo maeneo yote yatafikiwa na umeme kwa awamu.

Akijibu swali la Mbunge wa Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi (CCM),  aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme eneo la Dumila, Kilosa,  alisema Serikali kupitia TANESCO itatekeleza mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa Msongo wa Kilovoti 220 kutoka Morogoro hadi Dumila yenye urefu wa Kilomita 66 pamoja  na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme katika eneo la Magole – Dumila kupitia mpango wa Gridi Imara awamu ya pili unaotarajia kuanza mara tu baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza mwaka 2026.

Kuhusu Serikali kuimarisha Ofisi ya TANESCO Dumila ili iweze kutoa huduma bora, alisema kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma kwa wanachi ili waendelee kupata umeme wa uhakika.

Ameongeza kuwa, maelekezo ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ni kuhakikisha wafanyakazi wa TANESCO wanafanya kazi kwa weledi na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za umeme katika maeneo yote Tanzania.

Akijibu swali la Mbunge wa Mbinga Vijijini, Benaya Kapinga (CCM),  kuhusu ni lini Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme Wilaya ya Mbinga, Naibu Waziri Kapinga alisema mradi wa kituo hicho upo katika hatua za utekelezaji na unatakiwa kuanza awamu ya pili baada ya awamu ya kwanza kukamilika.

Aliongeza kuwa,  Serikali itausimamia mradi huo kwa weledi na nguvu ili uweze kukamilika na kuongeza kuwa Serikali imeboresha njia ya umeme ambayo inapeleka umeme kutoka Songea hadi Mbinga na laini za Mbinga Vijijini.

Vilevile, kuhusu swali la Mhandisi Mbunge wa Hanang’, Samweli Ayuma (CCM), ambaye alitaka kufahamu ni lini kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Hanang’ kitajengwa,  Kapinga alisema kipo katika awamu ya pili ya utekelezaji.

Google search engine

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here