Na MWANDISHI WETU
-DODOMA
SHIRIKA la Fedha la Kimataifa (IMF) litaipatia Tanzania zaidi ya dola za Marekani milioni 935.6, sawa na shilingi trilioni 2.46 ambapo kati ya fedha hizo, dola milioni 149.4, sawa na Shilingi bilioni 394.4 ni za kusaidia bajeti ya Serikali na kiasi cha dola milioni 786.2, sawa na shilingi trilioni 2.07 ni za kugharamia mpango wa miezi 23 wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia dirisha la Resilient and Sustainable Fund (RSF).
Taarifa ya uamuzi huo uliofikiwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo imetolewa kupitia tovuti rasmi ya Shirika hilo, Juni 20 2024 baada ya kumaliza mapitio ya tatu ya utekelezaji wa programu ya Extended Credit Facility-(ECF), inayohusisha upatikanaji wa mkopo nafuu kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa nchi kupitia sekta za uzalishaji na huduma za jamii kwa Tanzania.
Mnamo Julai 2022, IMF iliidhinisha jumla ya dola za Marekani bilioni 1.1, sawa na shilingi trilioni 2.4 kwa Tanzania.
Kukamilika kwa mapitio ya tatu ya Bodi hiyo, kumeruhusu Tanzania kupata mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 149.4, sawa na shilingi bilioni 394.4 na kunakamilisha rasmi Tanzania kupata fedha zote ambazo ni takribani dola za Marekani milioni 606.4 chini ya Mpango wa ECF.
Aidha shirika hilo limeiongezea Tanzania miezi sita ya utekelezaji wa mpango huo wa ECF hadi Mei 2026, ili kutoa muda wa kutosha katika kutekeleza na kutimiza malengo makuu ya mpango huo.
Waziri wa Fedha, Dkt Mwigulu Nchemba ameishukuru IMF kwa uamuzi huo wa kuridhia maombi ya Serikali kuhusu mpango huo baada ya majadiliano ya kina na yenye manufaa kwa Tanzania, hatua ambayo amesema itasaidia kwa kiasi kikubwa kusaidia utekelezaji wa Bajeti Kuu ya Serikali kwa kuwekeza fedha hizo katika Sekta za uzalishaji pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi.
Mwigulu ameahidi kuwa fedha hizo zitasimamiwa ipasavyo ili kukushukuru malengo ya upatikanaji wake kwa wanafunga ya wananchi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.