Na MWANDISHI WETU
-NAIROBI, KENYA
RAIS wa Kenya William Ruto amekataa kutia saini Mswada wa Fedha wa 2024.
Chombo cha habari nchini Kenya, Star Kenya kimeripoti kikinukuu vyanzo vya habari vya Ikulu kuwa Muswada huo utarejeshwa Bungeni kabla ya mapumziko ya leo Juni 26, mwaka huu.
Mkuu huyo wa nchi amependekeza marekebisho ya muswada huo ulioiddhinishwa na zaidi ya nusu ya wabunge, baada ya siku ya maandamano, ghasia na umwagaji damu, Rais wa Kenya William Ruto alihutubia Taifa kwa ujumbe wenye huzuni na wenye nguvu.
Alisema maandamano “halali” dhidi ya sera zake “yametekwa nyara na kundi la wahalifu waliopangwa,” alionya serikali yake itatumia njia zote ili kuzuia kujirudia kwa ghasia hizo, “kwa gharama yoyote”.
“Matukio ya leo yanaashiria hatua muhimu ya jinsi tunavyokabiliana na vitisho vya amani yetu. Tutahakikisha hali ya aina hii haijirudii tena,” alisema
Ujumbe wa Rais Ruto, ulikuwa jaribio la kunyakua udhibiti baada ya siku kadhaa za maandamano ya mitaani ambayo yameongezeka kwa nguvu. Siku ya Jumanne, waliongezeka huku watu wasiopungua watano wakipigwa risasi na mamia kujeruhiwa.
Lakini kwa muda mrefu baadhi ya watu wa Ruto lazima wahofu kwamba huenda mambo yasiwe rahisi sana, na kwamba bado kuna hatua ngumu za kuchukua siku za usoni.
Alipochaguliwa mwaka wa 2022 aliahidi kupunguza ufisadi, kuinua uchumi wa nchi unaodorora na kusaidia maskini, lakini Ruto sasa anakabiliwa na uasi usio na kifani dhidi ya muswada anaosema kuwa ni sehemu muhimu ya mpango wake wa kujenga Taifa.
Huenda ikawa rahisi kujua ni hatua gani angechukua iwapo upinzani anaokabiliana nao Ruto ungesalia ndani ya Bunge.
BUNGE LAKUBALI JESHI MTAANI
Bunge la Kenya limeidhinisha ombi la Baraza la Ulinzi la kutumiwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kutoa ulinzi kufuatia maandamano ya kupinga muswada wa Fedha kote nchini.
Kutokan na Waraka wa Amri ya ziada iliyopangwa jana Jumatano, hatua hiyo itaambatana na Kifungu cha 241 cha Katiba kinachohitaji kuidhinishwa na Bunge kabla ya wanajeshi kutumiwa kushughulikia masuala ya usalama wa ndani.
Hoja hiyo iliwasilishwa Bungeni baada ya ombi kutolewa na Baraza la Ulinzi siku ya Jumatano.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 241(3)(c) cha Katiba na vifungu 31(1)(b), 31(1)(c) na 32 vya Sheria ya Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Sura ya 199, Bunge hili linaidjinisha ombi la Baraza la Ulinzi la tarehe 26 Juni 2024 na, kwa maslahi ya usalama wa taifa, imeridhia kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kusaidia Huduma ya Kitaifa ya Polisi katika maeneo mbalimbali ya Jamhuri ya Kenya yaliyoathiriwa na maandamano ya ghasia yanayoendelea ambayo yamesababisha uharibifu wa miundombinu muhimu hadi hali ya kawaida irejeshwe,” ilieleza sehemu ya ilani hiyo