Na MWANDISHI WETU
-NAIROBI, KENYA
POLISI wa kupambana na ghasia wamefunga barabara karibu na Ikulu ya Nairobi katika juhudi za kuwazuia waandamanaji wa kupinga muswada ya fedha.
Polisi waliwazuia baadhi ya madereva na watembea kwa miguu wanaotumia barabara hizo.
Hiyo ilitokana na mwito wa kuandamana kupinga hatua ya Bunge kupitisha Muswada wa Fedha wa 2024, ambapo Rais William Ruto alikataa kutia saini mswada huo na kuwataka Wabunge kufuta vipengee vyote vilivyoleta mgogoro.
Mvua ndogo ilinyesha jijini Nairobi siku ya leo Alhamisi asubuhi lakini hilo halikuwakatisha tamaa polisi.
Barabara zilizoathirika ni pamoja na Dennis Pritt, State House Avenue, Processional Way, Valley Road, Jakaya Kikwete Road na zile zilizo jirani.
Waliwataka madereva wa magari na watembea kwa miguu kujitambulisha na dhamira yao kupita eneo hilo.
Wale wanaoishi karibu na hapo watakiwa kukaa ndani au kuondoka na kurudi jioni.
Polisi pia waliweka doria katikati mwa jiji na barabara kuu zinazoelekea huko kabla ya maandamano yaliyopangwa.
Waandamanaji hao walisema walipanga kuandamana hadi katikati mwa jiji ili miongoni mwa wengine kuomboleza waliouawa katika maandamano yaliyopita.
Biashara kuu zilibaki zimefungwa na kulikuwa na madereva wachache.
Polisi waliwahakikishia waliofungua biashara zao usalama wao.
Ripoti zinaonyesha polisi zaidi wa kupambana na ghasia walitumwa katika miji mikubwa nchini humo kabla ya maandamano hayo. Vizuizi zaidi viliwekwa kwenye barabara karibu na nyumba za kulala wageni za serikali.
Takriban watu 13 waliuawa Jumanne katika maandamano ya kupinga ushuru yaliyopendekezwa jijini Nairobi.