Na MWANDISHI WETU
-NAIROBI, KENYA
SHIRIKA la Fedha la Duniani (IMF) limesema linafuatilia kwa karibu matukio nchini Kenya, ambapo maafisa wa usalama wametuhumiwa kwa kuwapiga risasi waandamanaji wanaopinga Muswada wa Fedha wa mwaka 2024.
IMF imekuwa ikiitaka nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutekeleza mageuzi ya fedha ili kupata ufadhili muhimu.
“Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu matukio ya kusikitisha nchini Kenya katika siku za hivi karibuni. IMF inafuatilia kwa karibu hali ya Kenya,” imeeleza taarifa hiyo ya IMF
Taarifa ya IMF iliyonukuliwa na The Star ilisema. “Lengo letu kuu la kuunga mkono Kenya ni kuisaidia kukabiliana na changamoto za kiuchumi inayoikabili na kuboresha mpango wake wa kiuchumi na ustawi wa watu wake,” taarifa hiyo iliongeza kusema.
Kauli hiyo ilijiri saa chache baada ya Rais William Ruto kufuta mpango wa ukusanyaji kodi uliopangwa, baada ya kukabiliana shinikizo kutoka kwa waandamanaji.
WAKENYA WANAVYOKERWA NA MKOPO IMF
Tangazo la Shirika la Fedha Duniani IMF siku ya Ijumaa kwamba limeidhinisha mkopo wa Shilingi bilioni 255 au dola bilioni 2.34 kwa serikali ya Kenya limezua hisia kali kutoka kwa baadhi ya wakenya mitandaoni.
Wengi wameshangaa mbona IMF imeidhinisha mkopo huo ilhali tayari Kenya inazongwa na mzigo mkubwa wa madeni huku wananchi wakilalamikia ongezeko la gharama ya maisha.
Kero zao hizo walizitoa katika mitandao ya kijamii na hasa kwenye kurasa za akaunti za twitter na facebook za shirika la IMF.
IMF siku ya Ijumaa ilisema imekubali kuipa Kenya mkopo huo ili iweze kukabiliana na athari za kiuchumi za janga la Corona pamoja na kusawazisha mzigo wake wa madeni.
Isitoshe mkopo huo ndio wa pili chini ya mwaka mmoja ambao Kenya imepokea baada ya kupewa Shilingi bilioni 806 Mei mwaka jana .
Kenya imesema inalenga kuzitumia fedha hizo kupunguza makali ya janga la Corona kwa uchumi wake na pia kusawazisha madeni yake.