NA MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
KUPITIA Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Tanzania, yanayoendelea jijini Dar es Salaam, Benki ya NMB imeeleza ina uwezo wa kukopesha hadi Shilingi bilioni 515 kwa mkupuo mmoja ‘Single borrower limit’ kwa sababu yakufanya vizuri kwenye soko la Tanzania.
Hayo yamesemwa na Meneja wa NMB Tawi la Sabasaba, Kidawa Masoud, katika banda la benki hiyo kwenye Viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa, wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, na kwamba tangu Julai 2023 hadi Mei 2024, NMB imetoa mikopo ya zaidi ya Shilingi bilioni 585.
Alisema Benki hiyo inayo mizania wa zaidi ya Shilingi Trilioni 12.2, jambo ambalo unaowahakikishia uimara na uwezo wa kukopesha hadi Shilingi bilioni 515.
Uimara huo kiuchumi, unawapa uhakika wa kuendana na kasi ya Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeweka mazingira wezeshi kibiashara kama inavyoakisi kaulimbiu ya Maonesho ya Sabasaba mwaka huu; ‘Tanzania ni Sehemu Bora kwa Biashara na Uwekezaji.’
“Tuko imara kuhudumia kada zote za wateja wadogo, wa kati, wakubwa na mashirika ama kampuni, ambazo zinaweza kukopa kwetu hadi Shilingi bilioni 515 kwa mkupuo mmoja na nguvu hii inatokana na ongezeko la asilimia 26 ya Faida Baada ya Kodi tuliyopata mwaka 2023 ya Shilingi bilioni 542.
“Mpango mkakati tulionao kwa ni kuwafikia Watanzania wengi zaidi kupitia mifumo ya kidijiti, ambayo imeonesha mafanikio makubwa sana, kwani asilimia 94 ya miamala iliyofanyika kwa mwaka jana, imefanywa nje ya matawi 231 ya benki yetu kote nchini.
“Katika kufanikisha hili, tunazo akaunti za NMB Pesa zinazofunguliwa kwa Shilingi 1,000 tu, NMB Kikundi inayojumuisha wanachama wa vikundi mbalimbali vya kijamii, lakini pia tunao mkakati wa Huduma za Kibenki Vijijini ‘Rural Banking’ yenye lengo la kuvifikia vijiji 1,000 Tanzania,” alisema.
Kidawa alifafanua ya kwamba, ‘Rural Banking’ ni mkakati unaolenga kufungua akaunti milioni 1.5 kwa wakazi wa maeneo yasiyo na huduma za kibenki vijijini, kupitia mawakala wa benki hiyo waliotapakaa kila kona ya nchi.
Aidha, wakati kalenda ya Mwaka wa Fedha wa Serikali wa 2024/25 inayoanzia Julai 1, ikianza kutumika, NMB imetambia mafanikio katika makusanyo ya Mapato ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzaibar (SMZ), ilikofanyia maboresho mifumo yao na serikali zote.
“Mwaka huu tunaendeleza mashirikiano yetu na Serikali zote za Bara na Visiwani, katika kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato, ambako tumeweza kukusanya zaidi ya Sh. Trilioni 9.8 tangu mwaka 2018 kupitia NMB Wakala, NMB Mkononi na matawi yetu,” alisema Kidawa
Aliongeza ya kwamba, kama taasisi ya fedha kinara nchini, wanajivunia mafanikio yaliyowawezesha sio tu kutoa gawio kubwa zaidi la Shilingi bilioni 57.3 kwa Serikali ya Tanzania ambayo inamiliki asilimia 31.8 ya Hisa za Benki ya NMB, bali kutwaa Tuzo ya Benki Bora Tanzania kwa mwaka wa 11 mfululizo.
“Ni mwaka ambao tulipata pia Tuzo ya Benki Bora Tanzania tuliyopewa na Jarida la Euromoney, lakini pia tukapata idhini ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CSMA), kuwa wakala wa madalali wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).