Na MWANDISHI WETU
-DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), imeimwagia sifa Benki ya NMB kwa kukuza uelewa kuhusu elimu ya bima kwa jamii nchini.
Pia vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuisaidia Serikali kuibeba kwa uzito mkubwa ajenda hiyo ya kimkakati mbele ya Watanzania.
Akifungua mafunzo hayo kwa Wahariri wa vyombo vya habari, Naibu Kamishna wa TIRA, Khadija Said, amesema kuwa suala la Huduma za Bima Mtawanyo (BankAsuarance) ni muhimu likajulikana kwa jamii kwani ndio walaji wakuu wa huduma hizo.
Naibu Kamishna huyo ambaye alimwakilisha Kamishna Mkuu wa TIRA, amesema kuwa hatua ya kufanyika kwa mafunzo hayo itawawezesha washiriki kujua huduma mbalimbali kuitia mada zilizowasilishwa kama Bima ni nini, Benki Wakala wa Bima, Kazi za NMB katika uwakala, pamoja na huduma za kibenki na bima rafiki.
Amesema NMB imechukua hatua kubwa kwa kutenga muda wa kutoa elimu kwa wahariri na wanahabari waandamizi, ambao kwa kutumia vyombo vyao vya habari, wataongeza uelewa na elimu ya bima kwa jamii, ambalo ndio lengo chanya la Serikali.
“Mchango wa NMB ni mkubwa katika kukuza uelewa wa elimu ya bima kwa jamii, inachofanya hapa ni kutekeleza Mpango Mkakati wa Serikali na Mpango Mkakati wa TIRA, unaotaka kufikia mwaka 2030, asilimia 80 ya Watanzania wawe na elimu ya bima na asilimia 50 kati ya hao wawe wanatumia Huduma za Bima,” amesema
Pamoja na hali hiyo alisema kuwa miongozo ya BenkiBima (Bank Asuarance) imetolewa kwa mujibu wa Sheria, Kifungu cha 6(2) na Kifungu cha 11(A na B) ya Sheria ya Bima Sura ya 314, ambacho kinataka Mamlaka kuweka vigezo vya Bima vinavyopaswa kuzingatiwa na Taasisi za Fedha katika utoaji bima.
Khadija alikiri ya kwamba Benki Bima ni sekta inayokua kwa kasi nchini, ikihusisha Sekta ya Fedha na Sekta ya Bima yenyewe, siri ya ustawi na ukuaji huo sio tu suhirikiano baina ya taasisi hizo, bali pia mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kujenga na kuimarisha uelewa kwa jamii.
“Isaidieni Serikali kutangaza umuhimu na soko la bima kwa Watanzania, kwani bima ni jambo la msingi na muhimu zaidi, inalinda mali zetu dhidi ya majanga, inalinda afya zetu dhidi ya maradhi, inasaidia kusomesha watoto hata wazazi au walezi wanafariki, zaidi inaongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla,” amesistiza.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, amesema benki yake kama mdau wa maendeleo ya Watanzania, inatambua wajibu wao katika kusapoti juhudi za Serikali kuendeleza Sekta ya Bima Tanzania, ambalo ni moja ya vipaumbele vya taasisi yao.
“NMB ni kinara wa elimu ya hima kwa wananchi, uthibitisho ni leseni namba moja iliyopewa na TIRA kufanya uwakala wa bima, huduma iliyozaa Huduma ya NMB UmeBima na tunaamini kupitia mtandao wetu mpana unaojumuisha matawi 231, tutasaidia kwa haraka kukuza uelewa wa masuala ya bima kwa jamii.
“Tunajua wajibu na jukumu letu, hatuwezi kuliacha jukumu la kuelimisha Watanzania juu ya bima kwa Serikali pekee, na kwa kulitambua hilo, ndio maana sisi leo tumeanza kuliongezea uelewa na ufahamu kundi la wanahabari, ili wao waizungumzie elimu ya bima kwa mapana kupitia vyombo vyao.
“Serikali inajua kupitia TIRA ilikuja na sheria ambayo iliwezesha mabenki pia kuuza bima, tukiangalia kitakwimu, idadi ya Watanzania wanaoutumia bima au wenye uelewa wa masuala ya bima ni ndogo, sisi tunayo fursa pana ya kuisambaza kwa jamii ili wawe watumiaji halisi wa huduma hizo,” amesema.
Aliongeza ya kwamba, Sheria ya BankAsuarance ilikuja mwaka 2019, lengo likiwa ni kuifaidisha Sekta ya Bima kupitia mtandao mpana wa matawi ya taasisi za fedha, huku akisema kwa mfano NMB, imesaidia kuipeleka elimu hiyo katika kila wilaya, hata katika maeneo ambayo huduma za bima hakuna.
“Kwa hiyo sheria hii ikaja kuwezesjha kuisambaza huduma hii kwa jamii, kama tulivyosambaza matawi yetu na kweli imesaidia sana, kwani kwa sasa wananchi hawana tena haja ya kufika ziliko ofisi za bima, bali kwenye matawi yetu tu,” amebainisha Mponzi.
Alitolea mfano kwa kuyataja matukio ambayo jamii iliyokuwa na huduma za bima ilinufaika kupitia kampuni washirika wa bima kuwa ni moto ulioteketeza Soko la Kariakoo, Soko la Mlango Mmoja Mwanza, Wakulima wa Tumbaku Tabora, Mafuriko ya Hanang na wafanyabiashara wa masoko mbalimbali yaliyoteketea kwa moto.